• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Shujaa kuvaana na Fiji, Australia na Japan raga ya Los Angeles 7s

Shujaa kuvaana na Fiji, Australia na Japan raga ya Los Angeles 7s

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Shujaa watakaba koo na mabingwa mara mbili wa Olimpiki Fiji na mabingwa wa Raga za Dunia 2021-2022 Australia katika duru ijayo ya Raga za Dunia 2022-2023 nchini Amerika mnamo Februari 25-26.

Katika droo ya duru hiyo ya Los Angeles Sevens iliyofanywa Jumapili, Shuja pia italimana na Japan katika Kundi C.

Vijana wa kocha Damian McGrath wamekamilisha duru ya tano kwa pointi tano mjini Sydney, Australia. Wana jumla ya pointi 21 baada ya kupata moja mjini Hong Kong, tano (Dubai), tatu (Cape Town), saba (New Zealand) na tano (Sydney). Wameruka juu nafasi moja na kutulia nambari 12, wakisukuma Uhispania katika nafasi ya 13 kwenye ligi hiyo ya mataifa 15. Nambari 12, 13, 14 na 15 wote wanakabiliwa na hatari ya kutemwa katika ligi hiyo itakayokuwa na timu 12 msimu ujao. Inamaanisha kuwa Kenya ingali hatarini kutemwa. Hata hivyo, Shujaa wako pointi tatu nyuma ya nambari 11 Uruguay kwa hivyo wana matumaini makubwa ya kuponea shoka muradi wapate pointi nyingi katika duru zilizosalia mijini Los Angeles, Vancouver, Hong Kong, Singapore na Toulouse ambapo watakaotemwa watajulikana kabla ya msimu kukamilika mjini London.

Kuhusu Los Angeles Sevens ni kuwa mabingwa wa Singapore Sevens 2016 Shujaa itakuwa na kibarua kigumu kundini mwake. Imepoteza michuano 11 mfululizo dhidi ya Fiji, haijachapa Australia katika mechi tano zilizopita na pia imelemewa na Japan mara mbili mfululizo.

Mabingwa wa Sydney Sevens New Zealand wako Kundi A pamoja na washindi wa Cape Town Sevens Samoa, Amerika ya kocha Mike Friday na wageni Chile. Washindi wa Dubai Sevens Afrika Kusini, Ireland waliofika fainali mjini Dubai, washiriki wapya Uruguay na wenyeji wa Raga za Dunia 2021 Canada wametiwa Kundi B. Kundi D litakutanisha Ufaransa, Great Britain, Argentina na Uhispania.

Msimamo wa Raga za Dunia 2022-2023 baada ya Sydney 7s:

New Zealand (pointi 85), Afrika Kusini (76), Samoa (68), Ufaransa (68), Argentina (67), Fiji (67), Amerika (66), Australia (62), Ireland (58), Great Britain (35), Uruguay (24), Kenya (21), Uhispania (18), Canada (14), Japan (sita).

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Madai ya wizi wa kura yalishachunguzwa na...

Son Heung-min asaidia Tottenham kuingia raundi ya 16-bora...

T L