• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Simbas yalenga kurarua Zimbabwe Currie Cup

Simbas yalenga kurarua Zimbabwe Currie Cup

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Kenya Simbas wametaja kikosi chao tayari kwa mchuano wa daraja la kwanza Kombe la Currie dhidi ya Zimbabwe Goshawks utakaochezwa ugani Nakuru Athletic leo Jumamosi, Mei 20 kuanzia saa tisa alasiri.

Kocha Jerome Paarwater anakaribisha kikosini mzawa wa Fiji, Jone Kubu aliyekosa safari ya mwezi moja nchini Afrika Kusini ambapo Simbas walicheza mechi tano na moja nchini Namibia.

Katika mahojiano kuhusu mechi, Paarwater, ambaye ni raia wa Afrika Kusini, amekiri kuwa kibarua dhidi ya Goshawks kitakuwa kigumu.

“Zimbabwe wanapenda kutumia mchezo wa kukimbiakimbia kwa hivyo hatufai kuwapa mianya ya kufanya hivyo. Tulifungwa miguso rahisi dhidi ya Namibia wikendi iliyopita kwa hivyo pia lazima safu yetu ya ulinzi iwe macho,” ameongeza Paarwater.

Amefichua kuwa itakuwa muhimu Simbas kupata ushindi nyumbani.

Katika mechi zake nchini Afrika Kusini, Simbas ilipoteza dhidi ya Leopards na Boland Kavaliers bila ya kuingia uwanjani kwa kuchelewa kusafiri kutoka Nairobi.

Kisha, ilipigwa uwanjani na EP Elephants 18-7 na San Clemente Rhinos 33-22 na kupepeta Border Bulldogs 30-26.

Ilivuka mpaka hadi mjini Windhoek ambako ilipoteza 35-28 dhidi ya Namibia kabla ya kufunga safari ya kurejea nyumbani Mei 16.

Simbas itamenyana na timu kutoka Afrika Kusini Valke mnamo Mei 27 na SWD Eagles hapo Juni 3 ugani RFUEA mjini Nairobi katika mechi zake mbili za mwisho za kipute hicho.

Kikosi cha Kenya Simbas:

Wachezaji 15 wa kwanza

Ephraim Oduor, Griffin Musila, Hillary Mwanjilwa, Brian Juma, Hilary Odhiambo, George Nyambua (nahodha), Brian Ndirangu, Jeanson Musoga, Samuel Asati (nahodha msaidizi), Jone Kubu, Alfred Orege, Peter Kilonzo, Joel Inzuga, Beldad Ogeta na Ntabeni Dukisa;

Wachezaji wa akiba

Eugene Sifuna, Thomas Okidia, Wilhite Mususi, Hibrahim Ayoo, Elkeans Musonye, Brian Wahinya, Bryceson Adaka na Lameck Ambetsa.

Benchi ya kiufundi

Jerome Paarwater (kocha mkuu)

Jimmy Mnene (meneja wa timu)

Stephen Mankone (mnyooshaji wa viungo)

  • Tags

You can share this post!

Benki ya KCB yapiga jeki matayarisho ya Safari Rally kwa...

NDC ya Jubilee kuandaliwa uwanjani Ngong Racecourse

T L