• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
STAA WA SPOTI: Huyu fowadi Felix Ojow ni moto otea mbali Kenya Cup

STAA WA SPOTI: Huyu fowadi Felix Ojow ni moto otea mbali Kenya Cup

NA GEOFFREY ANENE

KLABU ya KCB imekuwa ikifanya vyema kwenye mashindano ya raga tangu 2015, ikiwemo kunyakua mataji matano ya Ligi Kuu (Kenya Cup) katika misimu saba iliyopita.

Mmoja wa wachezaji ambao wameifanyia kazi nzuri ni Felix Ojow.

Ameshinda Kenya Cup mwaka 2017, 2018, 2019 na 2021.

Vilevile, taji la Impala Floodlit 2017, 2018 2019 na 2022 akichezea wanabenki hao wa KCB walio na maskani yao katika uga wa KCB Sports Club mtaani Ruaraka, Nairobi.

Mzawa huyo wa Kaunti ya Nakuru alisomea shule ya msingi ya wavulana ya Baraka mjini Molo.
Alianza uchezaji wa raga akiwa kidato cha kwanza katika shule ya wavulana ya Utumishi Academy mjini Gilgil, mnamo 2009.

“Kutokana na umbo langu kubwa, nahodha wa Utumishi Academy, Leroy Anyembe, aliniamuru nifike uwanjani tayari kwa mazoezi tangu nilipowadia shuleni humo. Ndivyo nilivyoingilia raga,” alieleza Dimba.

Mshambulizi huyo anakumbuka jinsi alitatizika mazoezini siku za kwanza kwa sababu hakufahamu sheria za mchezo.

“Ilibidi meneja wa timu Reinhard Kipchoge anifunze kanuni hizo hata tukiwa kanisani misa ikiendelea,” anaongeza Ojow ambaye hucheza kama nambari saba (flanker).

Mzawa huyo wa Juni 1995 anakiri kwamba alichangamkia raga tangu alipoanza kuicheza.

“Sikupata pingamizi yoyote kutoka familia. Wameniunga mkono kwa hali na mali, na sasa pia mke wangu ameungana nao kunipa sapoti,” alisema Ojoo ambaye amefuzu kwa Shahada ya Biashara na Masuala ya Kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Baadhi ya manufaa ambayo ameona kupitia uchezaji wa raga ni kuzuru mataifa ya Namibia, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Uganda na Tanzania akiwa na timu ya taifa.

Alikuwa pia katika kikosi cha KCB kilichokita kambi ya mazoezi ya hali ya juu Afrika Kusini kwa mwezi mzima kabla msimu 2018-2019 kuanza.

“Kujishughulisha na raga pia kumenisaidia kujiepusha na maovu si haba ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, mtego ambao nimeshuhudia marika zangu wakinaswa humoa,” anahoji Ojow aliye na uzani wa kilo 105.

Akaongeza: “Raga pia imenisaidia kupata riziki. Mimi ni mhandisi wa kompyuta katika benki ya KCB.”

Ndoto yake ni kuchezea timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande Kenya Simbas.

“Nilichezea timu hiyo ila ya wachezaji walio chini ya umri wa miaka 19, almaarufu Chipu, kabla ya kuingia Homeboyz.

“Nimewahi kuitwa kikosini Simbas ingawa bado sijatumiwa katika mechi. Ndoto yangu ni kuchezea Simbas siku moja,” aeleza.

“Ningependa pia kuona mchezo huu ukikua zaidi na nipate kutumikia Shirikisho la Raga Kenya (KRU) kama mkurugenzi wa raga nitakapostaafu,” anasema.

Klabu ya KCB ilianzishwa 1989. Ilimsajili Ojow kutoka Homeboyz mwaka 2017.

Msimu huu wa 2022-2023 umesalia na mechi tano pekee kabla awamu ya muondoano ianze.

Umekuwa mzuri sana kwa KCB; wanaongoza ligi baada ya kushinda michuano saba mfululizo.

Ojow amechangia miguso minne. Alifunga hattrick wakati KCB — inayonolewa na Curtis Olago na Dennis Mwanja — ililipua Mwamba 82-10 mwezi jana 14 katika Chuo Kikuu cha Strathmore, Madaraka.

Pia, alipachika mguso katika ushindi wao wa 29-10 dhidi ya Homeboyz uwanjani KCB Ruaraka mnamo Desemba 10. Viongozi hao wa ligi watavaana na Monks ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) uwanjani Ruaraka, leo Jumamosi.

  • Tags

You can share this post!

VITUKO: Sogora King Kazu atachoka na mpira siku akifikisha...

Chelsea na Fulham watoshana nguvu kwa sare tasa katika...

T L