• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Thika Queens wafunga tatu bora KWPL huku Kisumu All Starlets ikipiga Kayole Ladies

Thika Queens wafunga tatu bora KWPL huku Kisumu All Starlets ikipiga Kayole Ladies

NA AREGE RUTH

MABINGWA watetezi Thika Queens walitamba nyumbani kwa mara ya pili mtawalia, walipowalima Kangemi Ladies 6-1 mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL), kwenye uwanja wa Manispaa ya Thika katika Kaunti ya Kiambu.

Kiungo Wendy Atieno ambaye anaongoza kwenye jedwali la wafungaji na mabao 10, alifunga bao moja dakika ya 48 kupitia penalti.

Sarah Chalovu alifunga mabao mawili dakika ya 27 na 49 sawa na kiungo Chris Kach ambaye alicheka na wavu dakika ya 17 na 50. Stellah Adhiambo alifunga kazi ya ziada dakika ya 52. Kwa sasa, Kach ndiye mfungaji bora wa pili na mabao saba.

Kangemi walipata bao la kufutia machozi kupitia Fablasi Atieno dakika ya 29. Baada ya kupoteza mechi hiyo, wako nafasi ya 11 na alama tatu.

Ushindi huo uliipelekea Thika kusalia nafasi ya tatu kwenye jedwali na alama 18 sawa na Gaspo Women ambao wameshikilia nafasi ya pili alama moja nyuma ya vinara Vihiga Queens.

Kwingineko, mabao ya  Elizabeth Muteshi na Stacy Koech katika dakika ya 18 na 90 mtawalia, yaliipandisha Nakuru City Queens hadi nafasi ya tatu baada ya kuinyeshea Trans Nzoia Falcons 2-0 katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo (ASK) mjini Nakuru.

Ugani KCB jijini Nairobi, Kisumu All Starlets walivuna ushindi wao wa pili mtawalia walipowavamia Kayole Ladies 4-0.

Mshambuliaji Monicah Etot alifunga hattrick dakika ya tatu na dakika za 34, 49 na 73. Kiungo Rosemary Oraro pia alifunga bao moja dakika ya 38.

Mshambuliaji wa Kisumu All Starlets Monicah Etot (mbele) akimzuia winga wa Kayole Starlets Suzan Awuor ili asichukue mpira wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) katika uwanja wa KCB jijini Nairobi mnamo Februari 12, 2023. PICHA | AREGE RUTH

Kocha wa Kisumu Juma Said alisema, “Ushindi huu umeleta motisha kwenye timu. Lengo letu ni kupata alama tatu kutoka kwa timu ambazo ziko mkiani kwenye jedwali ili tujiondoe kwenye hatari ya kushuka daraja.”

Kwa upande wa Kayole, nahodha wa timu hiyo Esther Mazira alisema kupoteza mechi zote tisa kunavunja moyo.

“Kwenye mechi yetu dhidi ya Kisumu, tulipata nafasi za kufunga ambazo hatukutumia vizuri. Tuna imani tunaweza kujitoa kwenye mtego wa kushuka daraja katika mechi zijazo za ligi. Tunarejea mazoezini kujipanga upya,” alisema Mazira.

Kisumu walipanda hadi nafasi ya tisa na alama 10.

Kayole kufikia sasa wamepoteza mechi tisa za ligi na wamesalia mkiani bila alama.

  • Tags

You can share this post!

Wapwani wakosoa serikali kukatalia minofu ya bandari

Bayern Munich wakomoa Bochum na kusalia kileleni mwa...

T L