• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Vihiga Queens wapigwa na Thika Queens katika KWPL huku Trans Nzoia Falcons wakiadhibu Kayole Starlets

Vihiga Queens wapigwa na Thika Queens katika KWPL huku Trans Nzoia Falcons wakiadhibu Kayole Starlets

NA AREGE RUTH

VIGOGO Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) Vihiga Queens, wamepata wakati mgumu mikononi mwa mabingwa watetezi Thika Queens ambao waliwanyoa bila maji 4-1 katika uwanja wa Manispaa ya Thika mjini Thika leo Jumapili.

Tangia kuanzishwa kwa timu hiyo mwaka 2013, Vihiga hawajawahi kufungwa mabao manne kwenye mechi ya ligi.

Kiungo wa Thika Wendy Achieng na Chris Kach walifunga mabao mawili kila mmoja. Achieng alijifunga bao na kuwazawadi Vihiga bao la kufutia machozi.

Kwa upande mwingine, Kayole Starlets walipoteza mechi yao ya saba mtawalia msimu huu kwa kukung’utwa 4-0 na Trans Nzoia Falcons uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi.

Kayole ambao walianza mchezo wakiwa wachezaji tisa uwanjani, waliadhibiwa na kiungo wa kulia Joyce Makungu ambaye alifunga hattrick dakika ya 13′, 57′ na 64′. Isitoshe, mshambuliaji Elizabeth Nafula pia alicheka na wavu mara moja dakika ya 33.

Baada ya kipigo hicho, kocha wa Kayole Joseph Sakwa anasema, baadhi ya wachezaji tegemeo hawakujitokeza kucheza mechi hiyo kutokana na sababu za ndani.

“Wachezaji  tegemeo walisusia kujitokeza jana. Hili lilichangiwa na kutokuwa na uhakika tungecheza mechi hiyo kutokana na changamoto za kifedha. Hali inazidi kuwa mbaya zaidi, lakini tunarejea nyumbani kufanya mazoezi kabla ya mechi ifuatayo,” alisema Sakwa.

Kwa upande wa Falcons, aliyekuwa kocha wa timu hiyo Justine Okiring amerejea tena kunoa makali ya timu hiyo. Amechukua mikoba ya aliyekuwa mkufunzi wa klabu hiyo Chris Mfede ambaye alitimuliwa mwezi Desemba 2022.

“Nilisafiri na wachezaji 13 pekee, hii ni idadi ndogo sana. Nilikuwa na wachezaji wawili tu wa ziada. Hali haijarejea kawaida kwa klabu ya Falcons baada yaliyotokea mapema mwezi huu Januari. Lakini ushindi huu umeleta motisha kwenye timu,” alisema Okiring.

Ugani Moi mjini Kisumu, Kisumu All Starlets walitoshana nguvu ya 1-1 dhidi ya Gaspo Women.

Bao la Kisumu lilifungwa na Treazer Manyala naye Jackline Nabangala akafungia Gaspo.

Mjini Nakuru, Nakuru City Queens walikaa ngumu kwenye mechi yao dhidi ya Gaspo Women kwa kuandikisha sare ya 1-1 katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo.

Stacy Koech alifungua ukurasa wa mabao na dakika ya 10.

Dakika sita baadae, kipa Juliet Adhimabo alipata kadi nyekundu dakika ya 16 baada ya kucheza visivyo.

Gaspo nao walipata bao la kusawazisha dakika za lala salama kipindi cha kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Ruto aokota waliotupwa na Uhuru

Magoha kuzikwa Februari 11 kwake Gem

T L