• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Ruto aokota waliotupwa na Uhuru

Ruto aokota waliotupwa na Uhuru

WASHIRIKA wa karibu wa Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta wanaoshikilia nyadhifa katika idara na mashirika ya serikali, wameingiwa na hofu Rais William Ruto akionekana kuongeza kasi ya kuwang’oa.

Rais Ruto amekuwa akitimua wandani wa Uhuru katika idara na mashirika ya umma na nafasi zao kuzijaza na watu waliotimuliwa na serikali ya Jubilee.Mwandani wa Rais Ruto wa hivi karibuni kutunukiwa wadhifa wa juu ni wakili Adil Arshed Khawaj ambaye Alhamisi alitangazwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya Safaricom.

Bw Khawaj alichukua nafasi ya Bw John Ngumi, mwandani wa Rais Mstaafu Kenyatta, aliyejiuzulu.Bw Khawaj aliondoka katika bodi ya Benki ya KCB mnamo 2020 baada ya kuhudumu kwa miaka minane.

Wakili huyo pamoja na Kairo Thuo, Wilson Kimutai Mugung’ei, Brenda Kokoi and Zipporah Kering mnamo 2020 pia walijiuzulu ghafla kutoka ukurugenzi wa kampuni ya kusambaza umeme, Kenya Power.

Lakini wadadisi wa masuala ya kisiasa walisema walitimuliwa na Rais Kenyatta kutokana na ukaribu wao na Naibu wa Rais Ruto ambaye wakati huo alitofautiana kisiasa na Kiongozi wa Nchi.

Bi Kering tayari ametunukiwa na Rais Ruto baada ya kuteuliwa na muungano wa Kenya Kwanza kujiunga na Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Kulingana na baadhi ya maafisa wakuu serikalini waliozungumza na Taifa Leo, wandani wa Uhuru wanaoshikilia nafasi za ukurugenzi wa mashirika ya umma na hata kibinafsi wamekuwa wakishinikizwa kujiuzulu badala ya kungojea kutimuliwa.

Bodi za mashirika ya umma na hata kampuni za kibinafsi zimekuwa zikisita kuongeza muda wa baadhi ya wakurugenzi wanaoaminika kuwa washirika wa Rais Kenyatta.

Mkurugenzi Mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa jana Jumamosi alilazimika kufafanua kuwa, angali anashikilia usukani wa kampuni hiyo ya mawasiliano ya simu baada ya kuzuka kwa tetesi kuwa alikuwa akikabiliwa na shinikizo za kumng’oa.

Bw Ndegwa alisema kuwa ana hakika kwamba ataruhusiwa na bodi kuendelea kushikilia hatamu ya uongozi Safaricom.

Wengine waliotimuliwa kutoka wadhifa wa uwaziri na Uhuru lakini wakatunukiwa nyadhifa za juu na Rais Ruto ni Davis Chirchir, Felix Koskei na mhandisi Michael Kamau.

Watatu hao waliohudumu katika baraza la kwanza la mawaziri wa Bw Kenyatta lakini wakatimuliwa mnamo 2015 baada ya wizara zao kutajwa katika kashfa za ufisadi.

Bw Chirchir, alikuwa waziri wa Kawi (wadhifa aliorejeshewa na Rais Ruto), Bw Koskei alikuwa Waziri wa Kilimo huku Mhandisi Kamau akihudumu kama waziri wa Barabara.

Watatu hao walitimuliwa baada ya kutajwa katika ripoti ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iliyowasilishwa na Rais Kenyatta Bungeni mnamo Machi 28, 2015 iliyoorodhesha maafisa 173 wa serikali kuu waliohusishwa na sakata kadha za ufisadi.

Bw Chirchir alituhumiwa pamoja na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Power Ben Chumo, kupokea hongo kupitia kampuni ya Windward Trading Ltd ili watoe zabuni.

Bw Chumo tayari ameondolewa mashtaka yote dhidi yake na duru serikalini zinasema kuwa huenda akatunukiwa wadhifa na Rais Ruto.Naye Bw Koskei ambaye mnamo Oktoba 14, 2022 aliteuliwa na Rais Ruto kama Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu na Mkuu wa Utumishi wa Umma, alijiuzulu mnamo Machi 28, 2015 kwa madai ya kuidhinisha uagizaji wa mahindi kinyume cha sheria. Baadaye, alijiwasilisha kwa EACC kuhojiwa lakini hakupatikana hatia.

Bw Kamau, alifutwa kazi na Bw Kenyatta kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka na ufisadi.Lakini kesi dhidi yake ikiwa bado inaendelea mahakamani, mnamo Desemba 23, 2022, Rais Ruto alimteua kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) kwa kipindi cha miaka mitatu.

Gavana wa zamani wa Kiambu, Ferdinand Waititu Babayao anapambana na kesi baada ya mashirika mbalimbali, kikiwemo Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kwenda kortini kupinga hatua ya Rais Ruto kumteua kuwa mwanachama wa Tume ya Kusafisha Mito jijini Nairobi.

Walalamishi wanasema kuwa, Babayao alibanduliwa afisini kabla ya kikamilisha muhula wake kama gavana wa Kiambu baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka hivyo hafai kushikilia afisi ya umma.

Akihutubu Desemba 7, 2022 katika mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alimsuta Rais Ruto kwa kuwateua watu aliowataja kama washukiwa wa ufisadi katika serikali iliyopita.

“Hii ni serikali ya wafisadi na watu ambao hawajahitimu kushikilia nyadhifa za umma,” akasema Bw Odinga.

Watu wengine waliotemwa wakati wa utawala wa Bw Kenyatta na kuokolewa na Rais Ruto kwa kutunukiwa nyadhifa za serikalini ni; aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Usambazaji Mafuta Nchini (KPC) Joe Sang’ aliyetimuliwa 2018 na Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta alitimuliwa wakati wa utawala wa Bw Kenyatta.

Wengine ni waliohudumu katika kitengo cha Habari za Rais (PSCU) James Kinyua, Eric Ng’eno, David Nzioka, Munyori Buku ambao walitimuliwa na Bw Kenyatta lakini juzi wakarejeshwa na Rais Kenyatta.Kesi za ufisadi na kutolipa ushuru dhidi ya Bi Wambui na Bw Kariuki ziliondolewa kufuatia kile kilichodaiwa kuwa ushawishi wa serikali.

  • Tags

You can share this post!

JAMVI LA SIASA: Maasi ya Raila ni ‘moto wa...

Vihiga Queens wapigwa na Thika Queens katika KWPL huku...

T L