• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Vishale: Wycliffe, Sakawa wakiri kupata upinzani mkali

Vishale: Wycliffe, Sakawa wakiri kupata upinzani mkali

Na JOHN KIMWERE

WYCLIFFE ‘Onetouch’ Omariba na Selina Sakawa warusha vishale mahiri nchini kitengo cha wanaume na wanawake mtawalia wanasema mchezo huo unazidi kuimarika.

Wawili hao wamefunguka hayo baada ya kila mmoja kushindwa kutetea ubingwa wao kwenye mechi za taji la Kiilu Cup zilizoandaliwa katika ukumbi wa Mid Kenya Establishment mjini Isiolo.

”Tunashuhudia ushindani mkali kwenye mashindano ya mchezo huu ambapo inaonekana itakuwa vigumu kwa mchezaji kushinda mataji mawili mfululizo,” Omariba aliyekuwa bingwa mtetezi wa taji hilo alisema.

Naye bingwa mtetezi kitengo cha wanawake, Sakawa alisema, ”Nimegundua wapinzani wangu wamejipanga kiume kudidimiza ubabe wangu mwaka huu.”

Kwenye mashindano hayo, Samwel Kuria wa Mang’ Darts aliibuka bingwa alipomshinda Leonard Kiwiri wa Stima kwa seti 5-4 katika fainali.

Ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa Kiwiri kutinga fainali za mchezo huo. Kitengo cha wanawake, kwa mara ya kwanza kabisa Risper Kurgat wa Magereza alitawazwa malkia wa kipute hicho ilipozoa seti 5-2 dhidi ya Ann Wairimu wa Rapid Deployment Unit (RDU).

Peter Muhia wa KETEWU aliibuka mchezaji bora kwa kuzoa alama 180 mara nne, huku Wilson Kaimenyi kutoka Meru akituzwa kwa kuvuna alama 141 akitumia mishale mitatu kwenye juhudi za kumalizia mechi zake.

Kwenye nusu fainali kitengo cha wanaume, Leonard Kiwiri alizaba David Gaitho wa Stima kwa seti 4-1 naye Samwel Kuria alivuna seti 4-2 dhidi ya Peter Muhia.

  • Tags

You can share this post!

Matokeo mseto yalishuhudiwa ya ligi za Kaunti na Kaunti...

Beki chipukizi anayelenga kufikia ubora wa Sergio Ramos wa...

T L