• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Beki chipukizi anayelenga kufikia ubora wa Sergio Ramos wa PSG

Beki chipukizi anayelenga kufikia ubora wa Sergio Ramos wa PSG

NA PATRICK KILAVUKA

ANASEMA nidhamu na mfumo wa uchezaji wa Sergio Ramos wa Paris Saint-Germain (PSG) ni kati ya mambo ambayo yamemchochea na kumtia motisha kusakata kandanda ili afikie kiwango cha kuchezea timu za hadhi nchini na ughaibuni.

Hata hivyo, aliongoza timu yake kunyakua taji la vipute.

Difenda na nahodha Emmanuel Mukene,16, ni mchezaji sasa wa timu ya wasiozidi miaka 17 ya WYSA United ambayo inahimiliwa na kocha Turncliff Asiebela na msaidizi wake Cornelius Chivoli iliyo na maskani yake uga wa Kihumbuini, Kangemi, Nairobi.

Ni mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Upili ya Tindiret,Kaunti ya Nandi, japo masomo ya msingi aliyapata Shule ya New Kihumbuini, Nairobi.

Ni kifunga mimba katika familia ya watoto wawili wa Bw Aloys Mukeni na Bi Virginia Wameria.

Alianza kuguza boli akiwa na miaka sita na aliichezea shule yake ya msingi hadi kiwango cha Kaunti ya Nairobi kabla corona kuvuruga shughuli za michezo.

Kwa kufanya mazoezi makali shuleni na nyumbani akiwa na timu mlezi United, ameona akifika hatua kwa hatua katika hatima ya kuwa mchezaji wa hadhi na kuchochea talanta yake ya soka kwa udi na uvumba.

Chini ya unahodha wake, walinyanyua taji la Westlands Soccer Associtaion la wasiozidi miaka kumi na mitano, 2020 baada ya kuwashinda watani wao Matrix 2-1 katika fainali iliyopigwa uwanjani Kihumbuini.

Anasema walicheza kwa umakini sana kwani wapinzani wao walikuwa wamejiamini kwamba wao ndio wangelibeba taji lakini mpira ukadunda.

Nahodha Emmanuel Mukene wa timu ya wasiozidi miaka 15 akinyanyua kombe la kipute cha Westlands Soccer Association. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Akiwa bado anafinyanywa katika timu hii, anasema mwanasoka mlinzi Alvin wa timu ya wazima, amekuwa kichocheo chake na alikuwa anamfuatilia katika mazoezi na kujifunza mawili matatu na yote tisa, kumi kuzamia katika kutia bidii ya mchwa kutetea timu yake na kujiimarisha.

“Hucheza kwa umakini na ni mstahamilivu sana akidhibiti washambuliaji jambo ambalo limekuwa likiweka ngome imara,” asema mwanadimba Emmanuel ambaye anayafanya mazoezi makali wakati huo wa likizo timuni wakishiriki katika michuano ya kirafiki pia.

Mbali na kocha Turncliff kuwapitia mawaidha na mbinu za uchezaji, difenda huyo wa pembeni, anasema mkufunzi huyo amekuwa akimtia mori ya kupigania timu kila uchao hususa yeye akiwa kapteni.

“Amekuwa akiongea na wazazi kila mara kwani kuna wakati nilipokuwa ninajiunga na timu, walikuwa wakikataa wakitaka nizingatie masomo, ” anadokeza Emmanuel na kuongezea kwamba, alishawishi kwa kina hali ambayo iliowapelekea kukubali aendelea kupiga soka.

Isitoshe, amekuwa akimhisani wakati mwingine na buti za kusakatia gozi.

Anasisitiza kwamba laiti hangekuwa mlezi huyo, hangejigundua zaidi kivipaji na kufika umbali huu. Mwanadimba huyu anawapongeza wazazi wake kwa kukubali aendeleze azma yake ya kupiga gozi na kuzidi kumuunga mkono. Pia, anamshukuru msaidizi wa kocha Chivoli kwa kumshikilia katika mazoezi.

Mwanasoka Emmanuel Mukene akipepeta mpira wakati akifanya mazoezi. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Anasema wakati alifurahia katika soka ni wakati walinyakua taji la Westlands Soccer Association na wakati walikwaruzana na Kibagare Sportiff ambayo inashiriki Ligi ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) na kutoka nyuma kisha kurambishana 3-3 katika mchuano wa kirafiki ambao ulikuwa mchezo mtamu na wa kusisimua.

Analo rai kwa wadau wa soka kwamba, waweke mikakati ambayo itaimarisha soka mashinani kwa kuwa na programu za kandanda na kuzifadhili akademia za kabumbu kama njia ya kuinua na kukuza vipaji chipukizi. Hii ni kwa sababu anaamini kuna vipawa mashinani na vinaozea tu mitaani!

Pili, kuwe na vipute vya kuanzia miaka ya chini kuimarisha talanta na maskauti na Shirikisho la Kandanda Kenya watembelea mashinani kugundua talanta.

Ushauri wake kwa wanasoka chipukizi ni kwamba, waendelea kucheza pasi na kukata tamaa, wawe na malengo katika soka na wayaafikie kwa kujitia mori ya kufanya mazoezi.

  • Tags

You can share this post!

Vishale: Wycliffe, Sakawa wakiri kupata upinzani mkali

Junet, Babu wadadisiwa na DCI

T L