• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Vita vya tatu bora KWPL ikiingia raundi ya 11

Vita vya tatu bora KWPL ikiingia raundi ya 11

NA AREGE RUTH

USHINDI wa Vihiga Queens dhidi ya Gaspo Women katika mechi ya raundi ya 11 ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) uwanja wa Mumias Sports Complex wikendi hii, utawafanya waendelee kusalia kileleni mwa jedwali.

Kikosi hicho cha kocha Boniface Nyamunyamu kinangoza kwenye msimamo wa ligi na alama 20. Gaspo wanashika nafasi ya tatu na pointi 19, wanaweza wakaingia kileleni mwa jedwali ikiwa watawaibisha wenyeji.

Mabingwa hao mara tatu wa KWPL, wamepoteza mara moja pekee nyumbani dhidi ya Ulinzi Starlets ambao waliwazaba 3-2 Ushindi mkubwa zaidi wa Vihiga wakiwa nyumbani msimu huu ulikuwa dhidi ya Kangemi Ladies walipowabomoa 12-0.

Kwa upande mwingine, katika mechi tano za mwisho za ligi ya ugenini Gaspo ameshinda mechi mbili dhidi ya Wadadia Women (3-1) na Ulinzi Starlets (2-0).

Walitoka sare mara mbili dhidi ya Kisumu All Starlets (1-1) na Bunyore Starlets (0-0) lakini wakaangukia kwa mabingwa watetezi Thika Queens (5-0).

Hata hivyo, Gaspo wamepata pigo kubwa baada ya kipa Pauline Kathuru kuvunjika mkono alipokuwa kazini dhidi ya Ulinzi.

Kocha mkuu wa Gaspo James Ombeng anasema, “Kathuru atakuwa nje kwa muda. Tunatazamia kuona jinsi tunavyoweza kutafuta fedha za kuhudumia operesheni yake.”

Thika wanashika nafasi ya pili kwenye jedwali wakiwa na alama 19. Mshambulizi wa Thika Wendy Atieno alifunga hattrick dhidi ya Kayole wikendi iliyopita, kwa sasa ndiye mfungaji bora akiwa na mabao 13 baada ya mechi 10. Atakuwa mchezaji wa kutazamwa sana katika uwanja wa GEMS Cambridge siku ya Jumapili, Thika itakabiliana na Zetech Sparks.

Kwenye mechi nyingine, Trans Nzoia Falcons wanatarajia matokeo chanya watakapomenyana na Kisumu All Starlets katika uwanja wa Ndura kaunti ya Trans Nzoia. Timu zote mbili zilisajili ushindi wa 1-0 wikendi iliyopita zilipomenyana na Bunyore Starlets na Zetech Sparks mtawalia.

Kiungo wa kutegemewa na Falcons Elizabeth Nafula atakuwa nje kwa mechi mbili baada kulishwa kadi nyekundu ya kumng’ata mpinzani wake wikendi iliyopita.

Baada ya ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Kangemi Ladies wikendi iliyopita, Ulinzi watakuwa tayari kuongeza ari yao kwani watakuwa wenyeji wa Kayole Starlets ambao wako mkiani.

Wikendi iliyopita Kayole walipata wakati mgumu mikononi mwa Thika ambapo walinyoroshwa 5-1. Kayole haijasajili ushindi wowote wala sare msimu huu. Wamepoteza mechi zote 10.

Kocha mkuu wa Ulinzi Joseph Mwanzia anasema ni lazima washinde hata baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo wakiwa nyumbani msimu huu.

“Tunamuheshimu mpinzani wetu licha ya nafasi aliyopo kwenye ligi. LIgi ina ushindani mkubwa, nitazungumza baada ya dakika 90. Mchezaji wangu tegemeo Joy Kinglady bado yuko nje anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, nitatumia wachezaji waliopo,” alisema Mwanzia.

Katika uwanja wa Nakuru Show Ground ulioko katika Kaunti ya Nakuru, Nakuru watakuwa wenyeji wa Bunyore Starlets huku Wadadia wakimaliza hatua ya wiki hii dhidi ya Kangemi Ladies katika uwanja wa Mumias Sports Complex.

  • Tags

You can share this post!

KIKOLEZO: Ifahamu hii sanaa ya ucheshi isiyo kawaida

BORESHA AFYA: Fahamu ni kwa nini unafaa kunywa chai ya...

T L