• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 7:50 AM
Waziri Namwamba aonya maafisa wasiofaa

Waziri Namwamba aonya maafisa wasiofaa

NA JOHN ASHIHUNDU

WAZIRI wa Michezo Ababu Namwamba amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali maafisa watakaopatikana na hatia ya kuwanyanyasa wanamichezo wakati wa kutekeleza majukumu.

Namwamba alisema jukumu la maafisa wa michezo ni kulinda na kusimamia vyema wanamichezo kisheria, huku akitoa onyo kali kwa maafisa hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sharia zilizowekwa na mashirika yao ya spoti.

“Hatutavumilia afisa yeyote atakayeendesha shughuli zake kinyume cha matakwa yake,kuambatana na sheeria iliyowekwa,” alionya.

Namwamba alisema hayo Ijumaa usiku huku akizikashifu vikali timu za Gor Mahia na AFC Leopards kutokana na matatizo yao ya mara kwa mara mikononi mwa FIFA na CAF.

Gor wiki hii iliondolewa kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF) kutokana na tatizo la kukosa kuwalipa wachezaji watatu ambao walikuwa wakiidai jumla ya Sh5 milioni.

Leopards nayo imeshtakiwa kwa FIFA kutokana na deni la Sh20 milioni la aliyekuwa kocha wao Patrick Aussems.

Adhabu kwa Ingwe ilijiri muda mfupi tu baada ya klabu hiyo kumaliza marufuku ya kutowasajili wachezaji kwenye vipindi tatu vya usajili.

Hii ni kutokana na deni ambalo pia walikuwa wakidaiwa na wanasoka wao wa zamani.

Namwamba ambaye alikuwa akizungumza Ijumaa usiku kwenye halfa ya kuwapa tuzo wanamichezo waliofaulu msimu uliopita alisema Serikali itabuni mbinu ya kuhakikisha kuwa timu hizo zote zinajiepusha na matatizo hayo.

Waziri huyo alitunuku Gor jumla ya Sh5 milioni kwa kushinda taji la 20 la KPL na kuiongezea Sh5 milioni ili wamalizane na madeni yanayowaandama.

Ingwe licha ya kutoshinda chochote msimu jana, walionewa imani na kupewa Sh5 milioni ambazo Waziri alisema zitawasaidia kupunguza deni la Aussems.

Pia kila klabu kwenye KPL ilituzwa Sh500,000 kama njia ya kuwaliwaza ikizingatiwa mara hii Shirikisho la Soka Nchini (FKF) halikuwa na chochote cha kuzitunuku timu.

“Sh5 milioni ambazo tumetoa kwa AFC Leopards na Gor tutatuma moja kwa moja kwa FIFA,” akasema Namwamba ambaye aliwakaripia vikali maafisa wa Gor kutokana na masaibu ambayo yalisababisha watimuliwe kwenye droo ya CAF.

“Rachier ambaye ni rafiki yangu angenijulisha kuhusu tatizo wakati bado kulikuwa na mwanya. Sasa hivi suala hilo limefungwa na hakuna chochote kile ambacho tunaweza kufanya,” akaongeza Namwamba.

Wakati wa tuzo hizo, Serikali ilitumia zaidi ya Sh100 milioni huku Namwamba akisisitiza kuwa Serikali ina ndoto ya kuinua michezo yote nchini kwa kuvutia wadhamini wa kigeni kuanzia msimu ujao.

  • Tags

You can share this post!

Azimio wakubali mazungumzo ya maridhiano na KK

Jombi atozwa Sh30, 000 kwa kugusa uchi wa mwanamitindo

T L