• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Yabainika De Bruyne aliumia jicho na kuvunjika pua wakati wa fainali ya UEFA kati ya Man-City na Chelsea

Yabainika De Bruyne aliumia jicho na kuvunjika pua wakati wa fainali ya UEFA kati ya Man-City na Chelsea

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata wa Manchester City, Kevin De Bruyne, alivunjika pua na kupata jeraha baya la jicho wakati wa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyowakutanisha na Chelsea mnamo Mei 29, 2021 jijini Porto, Ureno.

Nyota huyo raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 29 aliondolewa uwanjani katika dakika ya 60 na nafasi yake kutwaliwa na Gabriel Jesus baada kugongana na beki Antonio Rudiger wakiwania mpira wa hewani.

“Yasikitisha kwamba niliumia vibaya. Lakini nitapona hivi karibuni na kurejea ulingoni,” akasema De Bruyne ambaye huenda sasa akakosa kunogesha kampeni za Ubelgiji kwenye fainali zijazo za Euro kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

De Bruyne alijumuishwa katika kikosi kikosi kitakachotegemewa na Ubelgiji kwenye fainali hizo zitakazoshuhudia kikosi hicho nambari moja duniani kikishuka dimbani dhidi ya Urusi mnamo Juni 12 jijini St Petersburg, Urusi.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walikung’utwa 1-0 na Chelsea kwenye fainali ya UEFA kupitia bao la sajili mpya Kai Havertz aliyetua ugani Stamford Bridge mwishoni mwa msimu wa 2019-20 baada ya kuagana rasmi na Bayer Leverkusen ya Ujerumani.

Rudiger kwa upande wake, alitumia mtandao wa Twitter kufichua kwamba amekuwa akiwasiliana na De Bruyne tangu alipoumia huku akimtakia afueni ya haraka.

“Nasononeshwa na jeraha hilo. Bila shaka hakuna aliyekusudia tukio hilo. Nimezungumza tena na De Bruyne na ninamtakia nafuu,” akaandika beki huyo raia wa Ujerumani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KAMAU: Mageuzi yaja kwa viongozi wasaliti na wenye ubinafsi

Beki David Alaba ajiunga na Real Madrid bila ada yoyote