• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
BBI sasa ni mjeledi wa Ruto kutandika Azimio

BBI sasa ni mjeledi wa Ruto kutandika Azimio

NA WANDERI KAMAU

BAADA ya majaji wa Mahakama ya Juu kufutilia mbali Mswada wa Kurekebisha Katiba (BBI), Ijumaa, mswada huo sasa unaonekana kugeuzwa pigo la kisiasa kwa Rais Uhuru Kenyatta na muungano wa Kenya Kwanza.

Vigogo wa muungano huo sasa wametishia kuwashinikiza wabunge wao kuwasilisha mswada katika Bunge la Kitaifa, wakimtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya tathmini kubaini kiwango cha fedha ambazo zilitumika kufadhili shughuli za kuvumisha mswada huo.

Vigogo hao—Naibu Rais William Ruto, Musalia Mudavadi (ANC) na Seneta Moses Wetang’ula (Ford Kenya)— walisema kuwa ni lazima Wakenya wafahamu ukweli kuhusu kiwango cha fedha zilizotumiwa kuuvumisha mswada huo, walioutaja kama “njama ya viongozi wachache kujitengenezea nyadhifa za kisiasa.”

“Waziri wa Fedha Ukur Yatani na Katibu wake, Julius Muia, wana majibu makubwa ambayo lazima wawaeleze Wakenya. Wao ndio walitumika kutoa kibali cha kuidhinisha matumizi ya fedha hizo kwa mpango ambao kamwe haukuwafaidi Wakenya hata kidogo,” akasema Bw Mudavadi.

Kulingana na wadadisi wa siasa, kauli za vigogo hao ni mkakati wa “kuzidisha vita vya kisiasa” dhidi ya Rais Kenyatta kwa kutumia bunge.

Wanasema lengo lao ni “kulipiza kisasi” dhidi ya Rais Kenyatta, ikizingatiwa Rais vile vile amekuwa akitumia Bunge kuwaadhibu baadhi ya waandani wa Dkt Ruto.

“Kwa kuamua kuwatumia wabunge wao, lengo hasa la Dkt Ruto ni kulipiza kisasi dhidi ya baadhi ya waandani wake ambao waliondolewa kwenye kamati za Bunge na Seneti kwa kumuunga mkono. Lengo lake ni kutumia njia iyo hiyo kulipiza kisasi kwa

niaba yao, ikizingatiwa Rais amekuwa akiwatumia washirika wake katika bunge kuendesha baadhi ya ajenda zinazomfaa yeye mwenyewe dhidi ya wale waliokuwa wakipinga BBI,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Ili “kuitengenezea mapito” BBI, Rais Kenyatta aliuagiza uongozi wa Chama cha Jubilee (JP) kufanya mageuzi kwenye uongozi wa Bunge, Seneti na kamati za mabunge hayo mawili, kwa kuwaondoa watu walioonekana kuwa washirika wa karibu wa Dkt Ruto.

Baadhi ya viongozi waliotolewa ni aliyekuwa Kiongozi wa Wengi, Aden Duale (Garissa Mjini) na Kiranja wa Wengi, Bw Benjamin Washiali (Mumias Mashariki).

Nafasi ya Bw Duale ilichukuliwa na mbunge Amos Kimunya (Kipipiri) huku nafasi ya Bw Washiali ikichukuliwa na mbunge Emmanuel Wangwe (Navakholo).

Kwenye hotuba zake katika majukwaa mbalimbali, Dkt Ruto amekuwa akirejelea jinsi Rais Kenyatta amekuwa akiwahangaisha wandani wake kutokana na hatua yao kumuunga mkono kuwania urais Agosti.

Wadadisi pia wanataja hatua hiyo kama mkakati wa kujipigia debe kama viongozi “wanaomjali mwananchi.” Wanasema kwamba, ikizingatiwa msingi mkuu wa kampeni za vigogo hao watatu ni kufufua uchumi wa nchi, lengo lao ni kumsawiri Rais Kenyatta kama kiongozi mbadhirifu na asiyejali changamoto zinazowaathiri Wakenya.

“Kwenye kampeni zao, watatu hao wamekuwa wakiikosoa serikali kwa kuendesha miradi ambayo haiwafaidi Wakenya kwa vyovyote vile. Hasa, wamekita kampeni zao kwenye changamoto za kiuchumi na kiwango kikubwa cha deni la kitaifa. Hivyo, mpango wao ni kujisawiri kama viongozi wanaoijali nchi,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Hata hivyo, wadadisi wanataja mpango huo kutokuwa na athari zozote za kisiasa, ikizingatiwa Rais Kenyatta anaondoka ungozini.

  • Tags

You can share this post!

ODM yaahirisha uteuzi wawaniaji wakitishia kuhama

Kufeli kwa BBI pigo kwa Raila na Ruto

T L