• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:39 AM
Kufeli kwa BBI pigo kwa Raila na Ruto

Kufeli kwa BBI pigo kwa Raila na Ruto

NA CHARLES WASONGA

AILA KUZIMWA kwa mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) kumeonekana kuvuruga zaidi mpango wa ugavi wa mamlaka katika mirengo ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza.

Aidha, kuharamishwa kwa mpango huo kumeweka katika njiapanda wagombeaji urais wa mirengo hiyo miwili kuhusiana na suala zima la uteuzi wa wagombeaji wenza huku siku ya uchaguzi mkuu ikikaribia.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa sasa wanasema kuwa mgombeaji urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga na mpinzani wake mkuu Naibu Rais William Ruto (wa muungano wa Kenya Kwanza) watalazimika kuweka mikakati mipya katika safari zao za kuelekea Ikulu.

Mswada wa BBI ulikuwa umependekeza kupanuliwa kwa serikali kuu kwa kupendekeza kuundwa kwa nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.

Aidha, mswada huo ulitoa nafasi za kuteuliwa kwa baadhi ya mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge.

“Endapo, Mahakama ya Juu ingeamua mnamo Alhamisi kwamba mswada wa BBI ulikuwa halali ingekuwa rahisi kwa Bw Odinga na Dkt Ruto kupanga kambi zao kwa kuahidi wandani wao kutoka maeneo mbalimbali nyadhifa serikali,” anasema Bw Dismus Mokua.

“Hii ni licha ya kwamba marekebisho hayo ya Katiba yangefanyika baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, wala si sasa, kwa sababu kusingekuwa na muda wa kukamilisha mchakato huo,” mchanganuzi huyo anaongeza.

Kulingana na Bw Mokua, ingawa Dkt Ruto amekuwa akipinga mipango ya kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi serikalini, kuhalalishwa kwa uundwaji wa cheo cha Waziri Mkuu na manaibu wake wawili kungempa mwanya kuahidia baadhi ya wandani wake nyadhifa hizo.

“Aidha, Naibu Rais angeweza kunyamazisha kelele ndani ya muungano wa Kenya Kwanza kuhusu nafasi ya mgombeaji mwenza wake,” anaeleza.

Mgawanyiko umetokea ndani ya muungano huo kuhusu nafasi ya mgombeaji mwenza, wanasiasa wa Mlima Kenya wakishikilia kuwa nafasi hiyo ilitengewa eneo hilo.

Lakini wenzao, kutoka Magharibi ya Kenya, wakiongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, wanapendekeza kuwa nafasi hiyo ipewe kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.

Bw Mokua anasema kuwa mvutano kuhusu wadhifa huu ni ithibati tosha kwamba suala la ugavi wa mamlaka lina nafasi kubwa katika muungano wa Kenya Kwanza, kinyume na wanavyodai Dkt Ruto na vinara wenzake katika muungano huo.

“Ruto na wenzake wasiwadanganye Wakenya kwamba hawaongozwi na uchu wa mamlaka. Lengo la chama au muungano wowote huwa ni kutwaa mamlaka. Kwa hivyo kuhalalishwa kwa marekebisho ya Katiba na kubuniwa kwa nyadhifa zaidi kungemwezesha Dkt Ruto kuahidi wandani wake nyadhifa hizo,” anaeleza.

Kwa upande mwingine, kuhalalishwa kwa mswada wa BBI kungemfaa zaidi Bw Odinga katika juhudi zake za “kumtuliza” kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye inadaiwa anataka ateuliwe mgombeaji mwenza.

Vile vile, makamu huyo wa rais wa zamani ameripotiwa kudai kuwa chama chake kitengewe thuluthi moja ya nafasi katika serikali itakayoundwa na Bw Odinga endapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Duru ndani ya kambi ya kiongozi huyo wa ODM ni kwamba alitaka kuteua mgombea mwenza wake kutoka eneo la Mlima Kenya kama ishara ya kuonyesha shukrani kwa uungwaji mkono kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Kuharamishwa kwa BBI na majaji saba wa Mahakama ya Juu sasa kunamaanisha kuwa Bw Odinga atakuwa na kibarua kigumu kuteua mgombea mwenza. Aidha, sasa ana nafasi chache za kuwatunuku wandani wake, haswa magavana ambao wanahudumu muhula wa pili na wa mwisho,” anasema Bw Mark Bichachi.

Magavana ambao wamekuwa mstari wa kufanyia kampeni kama vile Hassan Joho (Mombasa) na James Ongwae (Kisii) ni baadhi ya wale wanaomezea mate nyadhifa kuu serikalini kwa sababu Katiba haiwaruhusu kuwania ugavana kwa mara nyingine.

  • Tags

You can share this post!

BBI sasa ni mjeledi wa Ruto kutandika Azimio

Mtihani mgumu kwa Orengo akilenga ugavana Siaya

T L