• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
ODM yaahirisha uteuzi wawaniaji wakitishia kuhama

ODM yaahirisha uteuzi wawaniaji wakitishia kuhama

NA WAANDISHI WETU

CHAMA cha ODM sasa kimelazimika kuahirisha uteuzi katika baadhi ya kaunti kufuatia malalamishi na vitisho kutoka kwa wawaniaji.

Chama hicho kinakumbwa na uasi wa ndani kwa ndani katika Kaunti ya Kisii kutokana na hatua ya Bodi yake Uchaguzi (NEB) kumpa tiketi ya moja kwa moja Mbunge Mwakilishi wa Kike Janet Ong’era.

Hatua hiyo imewakera zaidi ya wawaniaji 100 ambao wanalenga viti vya udiwani na ubunge. Wawaniaji hao wametishia kufika makao makuu ya ODM hapo kesho ili kujiondoa chamani iwapo uamuzi wa kumpa Bi Ong’era tiketi ya moja kwa moja hautabatilishwa.

Mwanzoni Bi Ong’era alikuwa ametangaza kuwa analenga kiti cha ugavana lakini mwezi uliopita, alighairi nia na kutangaza kuwa atatetea wadhifa wake.

Hasa hatua ya Mwenyekiti wa Bodi

ya Uchaguzi wa ODM Catherine Mumma kumpa tiketi ya moja kwa moja imemkashirisha mpinzani wake mkuu Dorice Aburi ambaye anaonekana kuwa kifua mbele katika kutwaa kiti hicho.

“Tumeshangazwa sana na habari kuwa Bi Ong’era amepokezwa tiketi ya ODM. Iwapo uamuzi huu hautabadilisha, sote tutaelekea makao makuu ya chama na barua zetu za kujiondoa ili tuwanie kama wawaniaji huru. Ni kama chama hakithamini demokrasia,” akasema Mbunge wa zamani wa Nyaribari Chache Chris Bichage.

Naye Naibu Spika wa Bunge la Kaunti ya Kisii, Davins Onuso alikashifu ODM kwa kurudia makosa ambayo ilifanya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017 ambapo iliwapa wawaniaji wasiomaarufu na kusababisha chama kikose kutwaa hata kiti kimoja cha ubunge katika kaunti hiyo.

Kupokezwa kwa Bi Ong’era tiketi

pia huenda kukamharibia hesabu mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati ambaye yupo kifua mbele katika kiny’ang’anyiro cha ugavana.

Chama hicho kiliahirisha uteuzi ulitarajiwa katika kaunti za Kilifi na Mombasa mnamo Jumanne na Jumatano wiki hii, ili kutoa nafasi kwa mashauriano zaidi kufuatia malalamishi kutoka kwa wawaniaji waliotisha kuhama.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya ODM, Catherine Mumma alifafanua kuwa uteuzi katika kaunti nyinginezo utaendelea kama kawaida.

“Uteuzi wa chama Kilifi na Mom – basa ambao ulikuwa umeratibiwa mnamo Aprili 5 na Aprili 6, umeahirishwa ili kupisha majadiliano na mashauriano,” ikasema sehemu ya taarifa ya Bi Mumma.

Japo Kilifi imekuwa ngome ya ki – siasa ya ODM na kinara wake Raila Odinga, mwaka huu inakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa chama cha PAA anachokiongoza Amason Kingi huku pia Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa pia akiegemea mrengo wa UDA.

Ruth Mbula, Maureen Ongala na Siago Cece

  • Tags

You can share this post!

Rais Kenyatta aomboleza babake Jaji Njoki Ndung’u

BBI sasa ni mjeledi wa Ruto kutandika Azimio

T L