• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 11:37 AM
Chebukati anaficha nini?

Chebukati anaficha nini?

CHARLES WASONGA Na BENSON MATHEKA

KATIKA kile Wakenya wengi wameanza kuchukulia kama hatua ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendesha shughuli zake kwa siri, tume hiyo imo mbioni kurudia makosa ambayo Mahakama ya Juu ilitambua na hatimaye kubatilisha matokeo ya urais 2017.

Hatua hiyo inatilia shaka kujitolea kwa tume hiyo chini ya kinara wake, Wafula Chebukati, kuendesha uchaguzi mkuu kwa njia huru na haki.

Wakati huo, mahakama ilisema uchaguzi sio matokeo pekee bali ni mchakato mzima kuendeshwa kwa uwazi.

Hata hivyo, siku 16 kuelekea uchaguzi mkuu ujao, IEBC inaonekana kuendesha shughuli zake kwa giza na kufanya wadau kutilia shaka maandalizi yake.

Licha ya wadau, wakiwemo wagombeaji, kuibua masuala kadhaa, ikiwemo uchapishaji wa karatasi za kura, kuhamishwa kwa wapiga kura kutoka baadhi ya vituo hadi upeperushaji wa matokeo, IEBC haionekani kuondoa hofu na kuzua maswali iwapo imejitolea kuziba mianya iliyotambuliwa na Mahakama ya Juu 2017.

Kukamatwa kwa raia watatu wa kigeni katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi jana Ijumaa, wakiwa na vibandiko vya kutambua vifaa vya uchaguzi kwa njia tatanishi kumethibitisha usiri ambao tume inaendesha shughuli zake.

Kinachofanya wengi kutilia shaka mchakato wa IEBC ni jinsi ilikosa kufahamisha maafisa wa usalama kuwasili kwa wahudumu hao huku ikiibuka kuwa kuna mgawanyiko miongoni mwa makamishna.

Baadhi yao wamekuwa wakilalamika kwamba, hawafahamishwi kuhusu hatua fulani ilipodhihirika shehena ya kwanza ya karatasi za kura ilipowasili nchini.

Duru zilisema baadhi ya makamishna hawakufahamu kuhusu kuwasili kwa karatasi hizo hadi saa chache kabla ya kutua katika uwanja wa JKIA.

Ingawa Bw Chebukati alilaani kukamatwa kwa watatu hao akidai walikuwa wafanyakazi wa kampuni ya Smartmatic iliyopewa kandarasi kuandaa vifaa vya kietroniki vitakavyotumika wakati wa uchaguzi, maswali yamezuka kuhusu anavyoweza kupuuza usalama wa vifaa muhimu vya kura.

Bw Chebukati hakuelezea ni kwa nini tume yake haikufahamisha usimamizi wa JKIA na asasi za usalama mapema kuhusu kuwasili kwa wageni hao.

Kulingana na utaratibu katika uwanja wa JKIA, maafisa wake hujulishwa kuhusu kuwasili kwa mizigo muhimu ya asasi za serikali mapema ili maandalizi ya mapema ya usalama yafanywe kuipokea.

Tukio la Alhamisi lilijiri siku mbili baada ya Bw Chebukati na maafisa wake kufeli kuwaonyesha wanahabari jinsi matokeo ya uchaguzi yatakuwa yakipeperushwa kutoka vituo 1, 111 visivyofikiwa na mtandao wa 3G au 4G.

Itakumbukwa kwamba mojawapo ya sababu zilizochangia Mahakama ya Juu kufutialia mbali matokeo ya urais 2017 ni kwamba, IEBC ilipeperusha matokeo kutoka vituo 11,000 bila kufuata utaratibu ulioko katika Sheria ya Uchaguzi.

IEBC pia ilidinda kuonyesha jinsi vifaa vya kieletroniki (KIEMs) vitakataa fomu 34A yenye dosari, ikisema kuwa “makarani wamefunzwa kufanya kazi inavyopasa”.

Kando na hayo, tume hiyo haijatoa rasmi ripoti ya ukaguzi wa sajili ya wapiga kura, ulioendeshwa na kampuni ya KPMG, licha ya shughuli hiyo kukamilishwa mwezi mmoja uliopita.

Hii ni licha shinikizo kutoka kwa maajenti wa wagombea urais wa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio.

Wiki jana, makundi ya mashirika ya kijamii pia yaliitaka IEBC kuweka wazi ripoti hiyo ili wadau na Wakenya kwa ujumla waikague.

  • Tags

You can share this post!

Wawaniaji Azimio wakimbilia Raila

Siasa: Maafisa waahidi kudumisha usalama Thika kukabiliana...

T L