• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:12 PM
Siasa: Maafisa waahidi kudumisha usalama Thika kukabiliana na magenge yanayohangaisha wawaniaji wa kike

Siasa: Maafisa waahidi kudumisha usalama Thika kukabiliana na magenge yanayohangaisha wawaniaji wa kike

NA LAWRENCE ONGARO

WANAWAKE wanaowania viti vya uongozi katika kaunti ya Kiambu wamelalamika jinsi wapinzani wao wanaume wanavyowatisha.

Bi Alice Ng’ang’a anayewania kiti cha ubunge Thika amesema uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na ushindani mkali ikilinganishwa na chaguzi za hapo awali.

Alisema hakuna haja ya wapinzani wao kutaka kuonyesha ubabe wao wa kimabavu kwani dakika ya mwisho ni mpigakura ndiye atakayetoa uamuzi wa mwisho.

Alitoa wito kwa vitengo vya usalama kufanya juhudi kuona ya kwamba wanawake wanalindwa – kutoka kwa wawaniaji wa vyeo vya juu vya ugavana hadi vile vya udiwani.

“Watu wanaotisha wenzao wa kike wanastahili kukabiliwa vilivyo kwani huo ni utovu wa nidhamu na hatua ya kisheria inastahili kuchukuliwa,” alifafanua Bi Ng’ang’a.

Alisema inasikitisha kuona vikundi vya vijana wakirarua picha za wagombeaji wa uongozi, halafu wanatoroka bila kutambuliwa.

“Tabia kama hiyo inastahili kukomeshwa mara moja na wahusika kutiwa mbaroni,” alisema Bi Ng’ang’a.

Bi Anne Mwikali Makobo ambaye pia anawania kiti cha ubunge cha Thika alisema majuzi genge la watu sita lilimfuata hadi kwake nyumbani majira ya usiku. Watu hao walimtolea vitisho.

“Mimi nilishtuka kuona kikundi cha watu wenye miraba minne wakija kwangu. Lengo lao nilijua lilikuwa ni kunitisha ili niwe na hofu na uwoga. Hata walitisha mama yangu mzazi,” alifafanua Bi Makobo.

Alisema baada ya kutundika picha zake katika maeneo tofauti “bado ninapata kuna watu wanazivizia usiku na kuzirarua.”

“Sisi wanawake tumebaki pweke kwani kufanya kampeni imekuwa ngumu ajabu,” alilalama Bi Makobo.

Alitoa wito kwa idara ya polisi kujitokeza wazi kuona ya kwamba hali inakuwa shwari nyanjani.

Bi Anne Wangari Wamugetha ambaye anawania kiti cha udiwani katika wadi inayofahamika kama Hospital Ward, mjini Thika, anasema watu wasiojulikana walivamia duka lake usiku wa manane na kulichoma ambapo vitu vyenye thamani kubwa viliteketea bila kutambulika.

“Licha ya kupitia masaibu hayo mimi bado nitaendelea na kampeni yangu lakini yote nimeMwachia Mwenyezi Mungu. Kama wahalifu hao walidhani wamenimaliza wajue kwamba Mungu ameniongeza nguvu zaidi,” alijitetea Bi Wamugetha.

Anaitaka serikali ifanye hima kunasa wezi hao ambao watalaaniwa hadi watakapotubu.

Baadhi ya wawaniaji viti vya ubunge na udiwani waliokongamana mjini Thika ili kutoa malalamiko yao kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwenye kikao ambacho maafisa kutoka idara ya polisi walihudhuria mnamo Julai 18, 2022. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Mkuu wa polisi mjini Thika Magharibi Bw Daniel Kinyua, baada ya kusikia malalamiko hayo yote aliwahakikishia wagombeaji wote kuwa kutoka siku hiyo Jumatatu, polisi watapiga doria saa 24 ili kukabiliana na vurugu zinazoweza kujiri.

Na alitoa wito kwa kila mmoja popote alipo hasa eneo la Thika kuhakikisha polisi wanafanya mikutano ya kila mara ili kujuliana hali.

Alitoa wito kwa wananchi kufanya juhudi kuona ya kwamba wanashirikiana na polisi ili kukabiliana na wahalifu.

  • Tags

You can share this post!

Chebukati anaficha nini?

Jaji na wakazi wa Kalimbini watishiwa kufukuzwa kutoka kwa...

T L