• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
‘Jicho Pevu’ kutetea ushindi wake kortini

‘Jicho Pevu’ kutetea ushindi wake kortini

NA BRIAN OCHARO

KESI ya kupinga ushindi wa mbunge wa Nyali Mohamed Ali katika uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 imewasilishwa katika mahakama ya Mombasa.

Bw Yassir Noor wa chama cha Jubilee anataka mahakama itupilie mbali ushindi wa Bw Ali akidai kuwa uchaguzi wa Agosti ulikumbwa na dosari nyingi.

Anaomba matokeo yafanyiwe uchunguzi kwa madai kuwa kulikuwa na udanganyifu. Pia , mwanasiasa huyo anataka kura za eneo bunge hilo lihesabiwe upya katika vituo vyote vya kupigia kura.

“Bw Ali hakuchaguliwa kihalali kuwakilisha eneo bunge hilo kwa miaka mitano ijayo,” alisema.

Aliomba mahakama katika ombi lake itoe tamko kwamba makosa ya uchaguzi ya aina ya uhalifu yalitokea katika eneo bunge hilo siku ya kupiga kuira Ameshtaki Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi na Bw Ali.

Anataka mahakama itumie busara yake kuagiza uchaguzi mdogo katika eneo bunge hilo akitaja utovu wa nidhamu katika uchaguzi uliokamilika.

Bw Ali ambaye alikuwa Mwanahabari wa zamani wa kampuni ya Standard Media alishinda kiti hicho baada ya kupata kura 32,988.

Bw Said Abdalla almaarufu Saido aliibuka wa pili kwa kura 18,642.

Wale waliowania kiti cha Nyali wamekataa matokeo ya uchaguzi huo.

Bw Ali alishinda wimbi la ODM kuhifadhi kiti chake kwa tiketi ya UDA.

Bw Abdalla aligombea kupitia tiketi ya ODM.Wengine walioshindwa katika uchaguzi wa Ubunge wa Nyali ambao wamekataa matokeo hayo ni mgombea huru Bw Eric Gitonga na Bi Millicent Odhiambo wa chama cha Wiper.

Wanadai kuchunguzwa kwa vifaa vya KIEMS ili kubaini ukweli wa matokeo ya kura za eneo bunge hilo.

Wamedai kuwa uchaguzi ambao Bw Ali almaarufu Jicho Pevu, aliibuka mshindi ulikumbwa na utovu wa nidhamu na hongo.

Walioshindwa wanadai kuwa wamebaini kuwa kura zilizopigwa katika eneo bunge hilo zilikuwa nyingi kuliko idadi ya wapiga kura waliojitokeza siku ya kupiga kura.

“Tulibaini kwa wasiwasi mkubwa kwamba maajenti wa chama cha UDA waliruhusiwa kuingia katika kituo cha kujumlisha kura huku wale wa vyama vingine wakiwekwa nje ili kuruhusu utovu wa nidhamu,” alisema Bw Abdalla katika mkutano wa awali na wanahabari.

  • Tags

You can share this post!

Raila asisitiza alidhulumiwa na IEBC, mahakama

Kampuni ambayo ilitapeli wasaka kazi yachunguzwa

T L