• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Jubilee sasa yashinikiza vyama vidogo vikunjwe

Jubilee sasa yashinikiza vyama vidogo vikunjwe

NA ONYANGO K’ONYANGO

CHAMA cha Jubilee sasa kimeanza mchakato wa kushawishi wandani wa Rais Uhuru Kenyatta waliokuwa wameunda vyama kuvivunja na kujiunga nacho.

Chama hicho kinachoongozwa na Rais Kenyatta kinafanya hivyo ili kuziba mianya katika ngome yake ambayo huenda ikasaidia kambi ya Naibu Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Aidha, Jubilee inasema hatua hii ni sehemu ya kampeni iliyoanza Januari 2022 ya kuifufua baada ya umaarufu wake kuyeyushwa na chama cha United Democratic Alliance (UDA), haswa katika ngome zake za Mlima Kenya na Rift Valley.

Hata hivyo, viongozi wa vyama vidogo vinavyoegemea mrengo wa Rais Kenyatta na ambao awali walilalamikia kutengwa na sekritariati ya Jubilee wamesema hawatafanya hivyo.

Viongozi hao ni Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui ambaye aliondoka Jubilee na kuunda chama cha Ubuntu People’s Forum (UPF). Wanasema walibuni vyama hivyo ili kuvitumia kama vyombo vya kupigania masilahi ya maeneo yao.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Gavana Kinyanjui pia alisema aliamua kuunda UPF kutokana na vita vya kila mara ndani ya Jubilee ambavyo vilihujumu demokrasia ndani ya chama hicho tawala.

“Kulikuwa na mivutano mingi ndani ya Jubilee ambayo nilihisi ilihujumu demokrasia ya ndani chamani. Hii ndio maana pamoja na wenzangu kutoka maeneo mengine tulianzisha chama cha kisiasa kwa jina Ubuntu Peoples’ Forum. Niliona kuwa hakukuwa na haja kwangu kusalia katika chama ambacho hakikuwa kikiendeleza masilahi ya watu wangu,” akasema Gavana huyo wa Nakuru alipokuwa akiunda UPF.

Gavana huyo alieleza kuwa UPF itadhamini wagombeaji katika viti vya udiwani, ubunge, mwakilishi wa kike, ugavana na useneta huku ikimuunga mkono Bw Odinga katika kiti cha urais.

Kufuatia kampeni mpya ya kufufua Jubilee ili kuiwezesha kudhamini wagombeaji kote nchini, chama hicho tawala sasa kinamshinikiza Gavana Kinyanjui na mwenzake wa Laikipia Ndiritu Muriithi kujiunga nacho.

Jubilee inawataka wawili hao kutetea viti vyao katika uchaguzi wa Agosti 9, kwa tiketi yake ili kufifisha nafasi UDA kupenya katika ngome zao.

Mkurugenzi wa uchaguzi katika Jubilee Kanini Kega jana alithibitisha kuwa wanajadiliana na viongozi ambao walikuwa wameunda vyama vingine kujiunga tena na chama hicho.

“Tunalenga sana Nakuru na Laikipia ili kuzuia makosa ambayo huenda yakachangia UDA kupata ushindi katika maeneo hayo,” akasema Bw Kega.

You can share this post!

Equity yalenga kubuni ajira faida ikipanda

Kivumbi cha udiwani cha Ichagaki chavua...

T L