• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Chama cha Jubilee chaanza kampeni kali ya kuvumisha Azimio La Umoja

Chama cha Jubilee chaanza kampeni kali ya kuvumisha Azimio La Umoja

Na LAWRENCE ONGARO

CHAMA cha Jubilee kimeanza kuvumisha Azimio La Umoja eneo la Gatundu Kaskazini.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bi Wanjiku Kibe, aliandamana na zaidi ya viongozi 10 kutoka maeneo tofauti ili ‘kufufua’ chama cha Jubilee huku pia wakitangaza ushirikiano wao na Azimio La Umoja.

Wakazi wa eneo hilo la Gatundu Kaskazini wapatao 5,000 walikongamana katika kituo cha kibiashara cha Ngorongo mnamo Ijumaa kwa lengo la kuhamasishwa kuhusu ushirikiano huo wa Jubilee na Azimio la Umoja.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ni Jude Njomo (Kiambu), Jonah Mburu (Lari), Jeremiah Kioni (Ndaragua), na Sabina Chege (Mwakilishi wa Wanawake, Murang’a).

Bi Kibe alisema watazidi kuhamasisha wananchi ili kuwapa mwongozo wa mwelekeo wanaostahili kufuata.

“Kwa muda mrefu wafuasi wengi wa Jubilee wamepotoshwa kuwa chama hicho kimesambaratika lakini hizo ni propaganda,” alifafanua Bi Kibe.

Alieleza kuwa serikali ya Jubilee ilizingatia kufanya kazi badala ya kupiga siasa, na wakati huu itaeleza wananchi mafanikio yake.

“Kwa mfano eneo la Gatundu barabara nyingi zineundwa, umeme kusambazwa na maji kuvutwa hadi vijijini. Kwa hivyo, wakati huu ni wa kueleza wananchi mafanikio yaliyoletwa na serikali,” alifafanua Bi Kibe.

Alihakikishia wafuasi wao kuwa wataanza kuingia mashinani hasa vijijini ili kueneza ‘injili’ ya Jubilee na Azimio la Umoja.

Mbunge wa Lari Bw Jonah Mburu alisema viongozi wa Mlima Kenya walio katika chama cha Jubilee wataingia mashinani kwa kishindo ili kuwarai wafuasi wao wafuate mwelekeo wa Rais Uhuru Kenyatta.

Wengi wa wafuasi waliohojiwa walieleza kuwa wataingia mashinani kutangaza ‘injili’ ya Jubilee na Azimio la Umoja.

Msisimko wa siasa umeanza kushika kasi huku sare nyekundu za Jubilee Party zikionekana mashinani.

  • Tags

You can share this post!

Voliboli: KPA, Kenya Army zatolewa kijasho

Wanjigi atisha kuzima ndoto ya Raila kuingia Ikulu

T L