• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:50 AM
Kakaye Joho akana kutumiwa na Ruto

Kakaye Joho akana kutumiwa na Ruto

Na WINNIE ATIENO

MWANASIASA Mohammed Amir, ambaye ni kaka mkubwa wa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, amepuuzilia mbali madai kuwa alijiunga na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ili kumsafishia njia gavana huyo kujiunga na Naibu Rais William Ruto.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Amir alisisitiza kuwa uamuzi wake kujiunga na chama hicho kinachoongozwa na Dkt Ruto, ulikuwa wa kibinafsi.

Tangu alipojiunga na UDA mwezi uliopita, kumekuwa na uvumi kuhusu ikiwa anatumiwa kumtafutia nafasi bora Bw Joho katika chama hicho.

Hii ni licha ya Bw Joho kusisitiza mara kwa mara kwamba hawezi kamwe kujiunga na Dkt Ruto kwani mitazamo yao kuhusu siasa na uongozi ni kama ardhi na mbingu.

Bw Amir alisema ikiwa kakake ataamua kujiunga na UDA, huo utakuwa ni uamuzi wake wa kibinafsi na kwa mtazamo wake itakuwa busara.

“Sijasikia kama ana mpango wa kuungana nasi lakini nadhani anafaa kuzingatia hilo. Ninajua watu wanashuku lakini ukweli ni kuwa niliamua kufuata kile ninachoamini moyoni mwangu,” akasema.

Alikiri kuwa uamuzi wake haujapokewa vyema na ameanza kutengwa na baadhi ya watu lakini hilo halitamtatiza katika safari yake ya kisiasa.

Kulingana naye, vyama vya ODM na Jubilee vilishindwa kutimiza matamanio ya wakazi wengi wa Mombasa, ndiposa akajiunga na UDA.

Bw Amir alisema vyama hivyo viwili vinavyoongozwa na Bw Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta mtawalia, havijasaidia kuboresha uchumi wa Mombasa licha ya kuwa Kaunti hiyo ina uwezo mkubwa wa kiuchumi.

“Kama kuna mtu yeyote ambaye haridhishwi na kiongozi yeyote wa UDA, shauri yao. Mimi sitaki kurithi uadui,” akasema.

Bw Joho ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM, ni miongoni mwa wanasiasa waliosimama kidete kutetea handisheki ya Rais na Bw Odinga, hatua ambayo iliwaudhi baadhi ya viongozi wa Pwani waliokuwa wandani wake.

Wakosoaji wake walilalamika kuwa, hatua hiyo ingeathiri ari yake ya kutetea maslahi ya Wapwani kwani kabla ya handisheki, alikuwa mstari wa mbele kupinga mambo yaliyoonekana kudhulumu eneo hilo, kama vile hitaji la kusafirisha mizigo inayotoka bandarini kwa reli ya SGR.

Hata hivyo, gavana huyo anayetumikia kipindi chake cha mwisho husema ushirikiano wa ODM na Jubilee, ulitoa nafasi kwa viongozi kushauriana na kutafuta suluhisho kuhusu matatizo hayo badala ya majibizano ambayo hayakuwa yakitoa suluhu zozote.

Bw Amir alisema nia yake kuwania useneta ni kuhakikisha kuwa utendakazi wa serikali ijayo ya kaunti utafuatiliwa kwa karibu hasa kuhusu matumizi ya pesa za umma.

“Siwanii nafasi hii kwa sababu ya jina la familia yangu bali nina nia ya kutumikia umma.”

Bw Amir, ambaye ni mkuu wa zamani wa idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa, anatarajiwa kushindania tikiti ya UDA dhidi ya Abdisalaam Kasim, Abdalla Miraji, Peterson Mitau, Charles Musyoka na Hamisi Mwaguya.

  • Tags

You can share this post!

Muungano wapendekeza adhabu kali kwa wazalishaji mbegu...

Uvumilivu ulivyompa Marionex fursa ya kufanya kazi na...

T L