• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:47 AM
Muungano wapendekeza adhabu kali kwa wazalishaji mbegu bandia

Muungano wapendekeza adhabu kali kwa wazalishaji mbegu bandia

Na SAMMY WAWERU

MUUNGANO wa watengenezaji na wafanyabiashara wa mbegu nchini (STAK) unalalamika kwamba wanaounda mbegu bandia huachiliwa kwa faini ya kiwango cha chini na mahakama, hali inayowachochea kuendeleza biashara hiyo haramu.

Chama hicho kinasema wahuni wahusika wanaopatikana na hatia na kufunguliwa mashtaka, wanaendeleza biashara yao hata baada ya kuachiliwa kwa kile wanataja kuchangiwa na “adhabu isiyowatikisa wala kuwashtua”.

Mwenyekiti wa STAK, Bw Kassim Owino ameonya endapo idara ya mahakama haitatathmini faini wanayotozwa baada ya kupatikana na makosa, huenda soko la pembejeo nchini likasheheni utapeli utakaokosa kudhibitika.

Alisema hatua hiyo itachangia kudorora zaidi kwa sekta ya kilimo, ambayo tayari inaendelea kulemewa na bei ghali ya pembejeo.

Gharama ya mbegu na fatalaiza imeongezeka kwa kiwango kikubwa chini ya kipindi cha miaka miwili iliyopita, wakulima wakilazimika kufukua mfuko.

“Faini inayotozwa wahusika wa mbegu bandia ni ya chini mno. Ni sawa na tone la maji kwenye ziwa,” Bw Owino akasema, akizungumza jijini Nairobi.

Mwenyekiti wa muungano wa watengenezaji na wafanyabiashara wa mbegu nchini (STAK), Bw Kassim Owino. PICHA | SAMMY WAWERU

Uzalishaji wa mahindi kwa mfano, visa vya wahuni kutia rangi punje za nafaka hiyo zilizovunwa zimeripotiwa suala ambalo linasababisha wakulima kutapeliwa. ‘Mbegu’ za aina hiyo zinashusha kiwango cha uzalishaji na ubora wa mazao.

“Baadhi wanabandika stika za Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) kwenye vipakio vya mbegu bandia,” Owino akaelezea.

Alisema STAK iko tayari kushirikiana na serikali ili kuimarisha ubora wa mbegu, katika mdahalo mzima kufanikisha sekta ya kilimo na ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi na ukuaji wa Kenya.

“Faini wanayotozwa ikiwa kidogo kuliko mapato wanayounda, hawataasi biashara hiyo haramu inayohangaisha kilimo,” akalalamika.

Akapendekeza: “Tunataka adhabu ambayo wakifikishwa kortini na kuhukumiwa, watajichuna skio na kutuma ujumbe wa onyo kwa mtandao wa wahusika wenza.”

Huku idadi kubwa ya wakulima nchini ikiwa ni ya wenye mashamba madogo, afisa huyo alisema wengi huwekeza katika mbegu na fatailaza na vilvile katika shughuli za upanzi, hivyo basi kuwepo kwa mbegu ghushi kunarejesha nyuma jitihada zao.

“Maisha ya wanaotegemea kilimo yanaathirika. Ni jambo linaloatua moyo wangu. Si sahihi, si haki kwa wakulima.”

Bw Owino alisema ni jukumu la muungano huo kwa ushirikiano na serikali kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zilizoafikia ubora wa bidhaa.

Kampuni zinazotengeneza mbengu nchi zimetakiwa kuhakikisha zimeweka kwenye vipakio vibandiko vya Kephis.

Taasisi hiyo ya serikali ndiyo imetwikwa jukumu kupitisha na kuidhinisha mbegu za mimea na nafaka nchini.

Aidha, stika za Kephis zina nambari za siri za mbegu zilizoafikia ubora wa bidhaa, ambapo mkulima baada ya kununua anatakiwa kukwaruza kibandiko na kuzituma kwa nambari iliyotolewa na shirika hilo kubaini ikiwa ni halali au bandia.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamuziki Koffi Olomide ahukumiwa kwa kupatikana na hatia...

Kakaye Joho akana kutumiwa na Ruto

T L