• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Kalonzo asisitiza lazima Sonko awe debeni Agosti 9

Kalonzo asisitiza lazima Sonko awe debeni Agosti 9

NA WINNIE ATIENO

KIONGOZI wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka amesisitiza kuwa gavana wa zamani wa Kaunti ya Nairobi, Bw Mike Sonko, atakuwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ugavana wa Mombasa licha ya kuzimwa na mahakama.

Bw Kalonzo aliwataka wakazi wa Mombasa wajitayarishe kwa kampeni kali pindi tu rufaa aliyokata Bw Sonko itakapomalizika.

Alisema haya baada ya Jaji Mkuu, Bi Martha Koome kuteua jopo la majaji watatu litakaloamua kesi ya mwaniaji huyo wa ugavana wa Mombasa kupitia chama cha Wiper.

Licha ya vita vikali vya kisheria dhidi ya mgombezi huyo, Bw Musyoka alielezea kuwa chama chake bado kitamsimamisha Bw Sonko.

“Bado tuna hamu ya kumrithi Gavana Hassan Joho na jopo hili la majaji watatu litatupa nafasi kama Wiper kufanya hivyo. Tutahakikisha kuwa tunampa Bw Sonko nafasi ya kupeperusha bendera yetu,” alisema Bw Musyoka alipokuwa akihudhuria harusi ya mwana wa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Fairdeal jijini Mombasa.

Tume ya Uchaguzi (IEBC) ilikuwa imemzuia Bw Sonko kuwania kiti hicho baada ya kubanduliwa uongozini. Kuzuiwa huku kulipelekea Bw Sonko kuwasilisha malalamishi kwa kamati ya kusuluhisha mizozo, ambayo ilishikilia uamuzi huo.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo, kamati hiyo ilikipa chama cha Wiper saa 72, kumchagua mgombea ugavana mwingine.

Wiper ilisita kumchagua mwaniaji mwingine na ikaelekea katika mahakama ya rufaa.

Wiki iliyopita, mahakama iliomba Jaji Mkuu, Bi Koome kuteua majaji watatu kusikiza kesi hiyo ya Bw Sonko.

Mgombea-mwenza wa Bw Sonko, Bw Ali Mbogo ambaye ni mbunge wa Kisauni, ana matumaini kuwa mahakama itatoa uamuzi utakaowapendelea.

Alieleza kuwa pindi tu uamuzi huo utakapotolewa, wataanza kampeni yao ya kusaka kura jijini Mombasa.

Bw Sonko alisema adui zao wanaendelea kuwakandamiza kupitia mahakama.

“Mikakati ya maadui zetu ni kwamba wanataka tuwe na shughuli nyingi mahakamani ili tupoteze mwelekeo,” alisema Bw Sonko kwenye mtandao wa Facebook.

Tayari kinyang’anyiro cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa, kina wagombeaji saba ambao IEBC imewaidhinisha kuwania ugavana.

Wagombezi hawa ni Daniel Kitsao ambaye ni mgombea huru, Hassan Omar wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Naibu Gavana, Dkt William Kingi wa Pamoja African Alliance (PAA), Hezron Awiti wa Vibrant Democratic Party (VDP), Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir wa Orance Democratic Movement (ODM) na Shafil Makazi wa UPIA.

  • Tags

You can share this post!

Raila alilia ngome yake isimwangushe uchaguzini Agosti

TAHARIRI: Viongozi wa siasa wawakumbuke raia wanaoteswa na...

T L