• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
TAHARIRI: Viongozi wa siasa wawakumbuke raia wanaoteswa na janga la njaa

TAHARIRI: Viongozi wa siasa wawakumbuke raia wanaoteswa na janga la njaa

NA MHARIRI

HABARI za Wakenya kuhangaishwa na baa la njaa zinaendelea kuripotiwa kutoka maeneo kadhaa nchini.

Mamilioni ya watu wakiwemo watoto na wazee wanalala njaa.

Hali iliyosababishwa na kiangazi cha muda mrefu katika maeneo hayo imezidishwa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Huku mamilioni ya Wakenya wakiwa katika tishio la kufariki kwa kukosa chakula, wanasiasa wanaogombea viti wanaendelea kutumia mamilioni kwenye kampeni zao katika maeneo hayo hayo.

Kinachosikitisha ni kuwa wanachowapa wakazi hao ni ahadi za kuwasaidia wakishinda uchaguzi mkuu ujao. Serikali, ambayo wanafaa kugeukia wakati wa janga inaonekana kuwasahau. Japo inadai imeweka mikakati ya kuzuia raia kufa njaa, juhudi zake zinaonekana kutozaa matunda na hali inaweza kuwa mbaya zaidi uchaguzi mkuu unaopisha serikali nyingine unapokaribia.

Afueni ambayo serikali imekuwa ikiahidi wahanga wa njaa huwa inachukua muda mrefu na katika hali ya sasa hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika kaunti zaidi ya 23 zinazokumbwa na kiangazi.

Inasikitisha, inahuzunisha na ikatamausha kuona hali ya wakazi wa Samburu, Kwale, Kilifi, Isiolo, Wajir, Turkana, Kitui na kaunti zingine wakikodolea kaburini kwa kukosa chakula, maji na dawa ilhali viongozi wao wanazama katika siasa.

Hata kama ni msimu wa kampeni za uchaguzi, serikali ingali mamlakani na wahanga wa njaa hawafai kusahauliwa. Kuna haja gani kusubiri watu wafariki ili serikali ipeleke chakula cha misaada?

Huu ndio wakati ambao serikali inafaa kuagiza na kuwezesha idara zote zinazohusika na ukame likiwemo jeshi la Kenya kuchukua hatua kuokoa raia wanaokumbwa na njaa. Juhudi ambazo zimekuwa zikiendelea zinafaa kupigwa jeki kama jambo la dharura. Viongozi wanaotafuta viti kwenye uchaguzi mkuu ujao pia wanafaa kufahamu kuwa ukame ni tisho kwa maendeleo ya nchi wanayoahidi kustawisha wakiingia mamlakani.

Nizike nikiwa hai ni msemo unaoafiki wakati huu kwa kuwa ikiwa viongozi hao hawawezi kuwasaidia wanaokumbwa na njaa kama jambo la dharura, itakuwa vigumu kuwasaidia wakiingia mamlakani.

Wakati umefika Wakenya kuungana kuwasaidia wenzao kwa kuchanga walichonacho jinsi ambavyo walikuwa wakifanya miaka iliyopita lakini pia kufanya hivi, uongozi unahitajika.

You can share this post!

Kalonzo asisitiza lazima Sonko awe debeni Agosti 9

TALANTA: Wanahabari chipukizi

T L