• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Kingi asema ameanza harakati ya kujiondoa katika Azimio

Kingi asema ameanza harakati ya kujiondoa katika Azimio

NA WINNIE ATIENO

CHAMA cha Pamoja African Alliance, kinachohusishwa na Gavana wa Kilifi, Amason Kingi, kinapania kujiondoa kwenye muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya kikidai kinaonyeshwa madharau.

Wakuu wa chama hicho wamemwandikia barua rasmi Msajili wa Vyama, Bi Anne Nderitu wakimuomba kujiondoa kwenye muungano huo unaompigia debe kinara wa ODM, Bw Raila Odinga kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Gavana Kingi alisema anapania kujiondoa kwenye muungano huo.

“Tunathibitisha kuwa tuliandika barua mnamo, April 25 kwa msajili wa vyama tukitaka kujiondoa kwenye muungano wa Azimio la Umoja One Kenya,” alisema Gavana Kingi kwenye anwani yake ya Twitter.

Hata hivyo, Bw Kingi ambaye anamaliza hatamu yake ya ugavana wa mihula miwili alikana madai kwamba PAA inapania kujiunga na muungano unaompigia debe kinara wa UDA, Bw William Ruto wa Kenya Kwanza.

Katika barua rasmi kwa msajili wa vyama, PAA iliomba kujiondoa katika muungano huo ikisema inafichwa mambo mengi ya chama.

Baadhi ya wakuu wa chama hicho walitoa mfano wa baraza lililobuniwa majuzi ambapo hakuna mkuu wa PAA ambaye aliteuliwa.

Waliiambia Taifa Leo kwamba wanapitia maonevu chamani.

“Eneo la Pwani tuliona majina ya kina Gavana Hassan Joho, wabunge ni pamoja na Naomi Shabaan (Taveta) na Mishi Mboko (Likoni) lakini hakuna mahala ambapo mmoja wetu aliteuliwa. Hatujachukuliwa kama mmoja wao ilhali tuliunga muungano wao,” alisema Mwenyekiti wa kitaifa wa PAA Bw Ibrahim Babangida.

Bw Babangida alisema pia PAA haijwai kuonyeshwa mkataba waliotia saini walipoungana na Azimio La Umoja One Kenya.

“Heshima ni muhimu sana katika siasa. Hakuna chama ndogo wala kubwa zote ni sawa na tunahitaji kuhehsimiwa kama wengine. Lakini kujiondoa kwetu haimaanishi tunaenda kujiunga na Kenya Kwanza, hizo ni porojo. Lakini tutaongea na mtu yeyote ambaye atatupa heshima yetu tunayostahili,” alisema.

Kwa sasa, PAA inaendeleza shughuli zake za kusaka ungwaji mkono na kuhakikisha wanazoa viti vyote vya kisiasa kuanzia za wawakilishi wa wadi, wabunge, maseneta na magavana.

Bw Babangida alisema kwa sasa hawajaamua watamuunga mgombea yupi mkono kwenye urais.

Huko Kilifi wakili George Kithi atapeperusha bendera ya PAA huku Bw Lung’anzi Mang’ale naye akipewa cheti cha Kwale.

You can share this post!

Kalonzo motoni kusukuma Sonko

Sababu ya mizinga 19 kufyatuliwa badala ya 21

T L