• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Kimunya apuuza waundao vyama vidogo Mlimani

Kimunya apuuza waundao vyama vidogo Mlimani

Na WAIKWA MAINA

KIONGOZI wa wengi katika Bunge la Kitaifa, Amos Kimunya, ametofautiana na magavana wa eneo la Kati mwa Kenya kuhusu wazo lao la kukumbatia vyama vidogo badala ya kuwa na muungano wa kisiasa wa eneo hilo.

Bw Kimunya alisema katika kazi yake kama kiongozi wa wengi ameng’amua kuwa Kenya haihitaji vyama vidogo kwani ni vigumu kushawishi wabunge wa vyama hivyo kuunga mkono ajenda ya serikali bungeni.

“Unalazimika kuwapigia simu viongozi wengi wa vyama ilhali baadhi ya vyama hivyo huwa na wabunge wachache mno. Vile vile, inakulazimu kuwapigia simu maafisa wengine wa vyama hivyo ambao huwa wasumbufu. Kwa hivyo inakuwa kazi ngumu kusukuma miswada na hoja za serikali bungeni,” akasema.

Akiongea katika soko la Gathiriga eneobunge la Kipipiri ambako aliungana na Waziri wa Maji Sicily Kariuki kuzindua mradi wa maji, Bw Kimunya alisema eneo la Kati litasalia ndani ya Jubilee.

“Na tutawahimiza wagombeaji wote kuwania kwa tiketi ya chama hiki cha Jubilee. Rais Uhuru Kenyatta bado ndiye kiongozi wa chama chetu na wale ambao wanaongea kuhusu vyama vingine wanaota. Tutasalia mahala ambapo Rais yupo na kuendelea kuvumisha Jubilee huku tukipanga kutetea viti vyetu kwa tiketi ya chama hicho,” akasema Bw Kimunya.

Kiongozi huyo wa wengi bungeni alisema ana uhakika kwamba wagombeaji wa Jubilee watashinda viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Aliahidi kwamba hivi karibuni ataanzisha kampeni kali ya kuvumisha Jubilee katika maeneo yote ya Mlima Kenya na taifa kwa ujumla.

Baadhi ya magavana wanachama wa Muungano wa Kiuchumi wa Eneo la Kati wiki jana waliahidi kuunda muungano wa kisiasa ambao utaendeleza masilahi ya eneo hilo na kupalilia umoja miongoni mwa viongozi.

Wakiongozwa na Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia, magavana hao; Nderitu Muriithi (Laikipia), James Nyoro (Kiambu), Lee Kinyanjui (Nakuru) na Mutahi Kahiga wa Nyeri walisema ipo haja wao kuunga mkono vyama vyenye mizizi katika eneo la Mlima Kenya.

Hii ni iwapo Jubilee haitafanyiwa ukarabati ili irejelee umaarufu wake wa zamani.

Hata hivyo, Bw Kahiga amejiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Tayari Bw Muriithi ameanza kuvumisha chama cha PNU ilhali Bw Kinyanjui na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi wamesajili vyama vyao vinavyounga azma ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ya kuingia Ikulu 2022.

You can share this post!

Kananu ageuzwa ‘gavana kinyago’ mbele yake Uhuru

Wagombeaji ugavana Homa Bay wakimbilia koo kujitafutia...

T L