• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Karua atambuliwa kwa misimamo thabiti kuhusu utawala wa kisheria

Karua atambuliwa kwa misimamo thabiti kuhusu utawala wa kisheria

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Narc-Kenya, Martha Wangari Karua ni mwanasiasa anayetambuliwa kwa misimamo thabiti hasa kuhusu utawala wa kisheria na haki.

Akiwa mbunge wa Gichugu mnamo Juni 16, 2001, Bi Karua alishangaza wengi kwa kuondoka katika mkutano wa harambee ulioongozwa na Rais Daniel Moi walipotofautiana hadharani.

Bi Karua, aliyekuwa akihudumu muhula wa kwanza katika bunge, alionyesha ujasiri wa kipekee kwa kuondoka katika uwanja wa Kerugoya wakati Moi alikuwa akihutubu.

Hii ni licha ya kuwa Moi alijulikana kwa kukabili vikali waliomkosoa.

Bi Karua alisema aliamua kuondoka kwa kuwa hangevumilia kauli za washirika wa Moi za kudharau upinzani.

“Kila wakati katika mikutano ya hadhara Moi hakuwa akitambua viongozi wa upinzani, na ndiyo sababu niliondoka katika mkutano wake Kirinyaga aliponinyima nafasi ya kuhutubia wakazi,” Bi Karua alisema kwenye mahojiano mwaka 2021.

Katika tukio lingine aliloonyesha msimamo wake alipojiuzulu kama waziri wa Haki na Masuala ya Katiba mnamo Aprili 6, 2009 baada ya kutofautiana na serikali ya Rais Mwai Kibaki.

Wakati huo, Bi Karua alisema alikuwa akihujumiwa katika kazi yake, jambo ambalo hangevumilia.

Alitoa mfano wa tukio ambapo Kibaki aliteua majaji bila kumfahamisha ilhali alikuwa waziri mhusika.

Mwaka 2021 Bi Karua alikuwa mmoja wa mawakili waliopinga mchakato wa BBI ulioanzishwa na Rais Uhuru Kenya na Raila Odinga akisisitiza kuwa ulikuwa unahujumu Katiba iliyopitishwa 2010.

Mchakato huo ulizimwa na korti kwa juhudi za Bi Karua na watetezi haki wenzake.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wazazi wakomeshwe kupeleka watoto kwa mikutano ya...

Kwa kuteua Karua, Raila alenga kura za wakazi wa Mlima...

T L