• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 12:05 PM
Kiraitu atwaa uongozi chama kipya Mlimani

Kiraitu atwaa uongozi chama kipya Mlimani

KENNEDY KIMANTHI na GITONGA MARETE

GAVANA wa Meru Kiraitu Murungi amethibitisha nafasi yake kama mfalme wa mabadiliko mapya kisiasa baada ya kupata idhini ya kuchukua usukani wa chama cha Restore and Build Kenya (RBK).

RBK sasa itabadilishwa jina na kuanza kuitwa Devolution Empowerment Party (DEP) ambayo huenda ikatumika kama chombo cha kisiasa kwa eneo la Mlima Kenya Mashariki linalojumuisha kaunti za Meru, Embu na Tharaka Nithi.

Tayari, Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Anne Nderitu, ameidhinisha jina hilo jipya na alama ya Basi, iliyokuwa ikitumiwa na chama cha Bw Murungi kilichosambaratika cha Alliance Party of Kenya (APK).

Gavana Murungi amekuwa akishiriki kila uchaguzi kwa kutumia chama kipya tangu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ulipoanza Kenya 1992.

Iwapo atatetea kiti chake kwa kutumia chama kipya, ataandikisha rekodi mpya katika historia ya vyama vya kisiasa nchini.Aliingia kwa kishindo kwenye ulingo wa siasa kwa kushinda kiti cha ubunge cha Imenti Kusini mnamo 1992 kupitia Ford-Kenya lakini akahamia Democratic Party cha Bw Mwai Kibaki katika uchaguzi wa 1997 na kutetea kiti chake.

Mnamo 2002, Bw Murugi alitumia chama cha NARC kushinda kiti hicho cha ubunge kwa mara nyingine lakini akashiriki uchaguzi wa 2007 kwa kutumia tiketi ya chama kipya cha Party of National Unity (PNU).

Alishinda kiti cha Useneta Meru mnamo 2013 kupitia Alliance Party of Kenya (APK) ambapo 2017, alishinda kiti cha ugavana kupitia tiketi ya Jubilee Party, chama alichochangia mno uundaji wake lakini ambacho kwa sasa kimetangazwa kama “kilichokufa na kuzikwa.”

Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa lilitupa kesi iliyowasilishwa na wanachama wawili wa RBK wanaopinga hatua ya kubadilisha uongozi na jina la chama hicho.

Kufuatia uamuzi huo, kundi la wanasiasa kutoka Mlima Kenya Mashariki wakiongozwa na Gavana Murungi, sasa wamechukua usukani kamili wa chama hicho ambacho aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Elimu, James Kiyiapi, alitumia kugombea urais 2013.

Bw Murungi, Ijumaa aliwapuuzilia mbali wanasiasa wanaopinga hatua yake ya kubuni chama cha kimaeneo, akisema chama chake kipya kitakuwa na ushawishi mkuu katika Uchaguzi Mkuu 2022.

Alisema kufuatia kutupiliwa mbali kwa kesi na jopo linalosimamia vyama vya kisiasa, chama hicho kipya kitazinduliwa hivi karibuni ili kusimamia shughuli za kisiasa eneo hilo.

“Chama chetu ndicho kitakachofanya majadiliano kwa niaba ya eneo hili. Wakati wanaume wengine katika ODM, Wiper, Ford Kenya, Kanu na ANC watakapoketi kwenye meza kujadili jinsi ya kugawanya raslimali za kitaifa, pia sisi tutakuwepo hapo,” alisema.

You can share this post!

Mozzart yapiga jeki Harambee Stars kwa Sh3 milioni kucheza...

Karugu ataka madiwani wazuiwe kumtimua ofisini