• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Kisasi: Waliopinga KK waanza kukiona

Kisasi: Waliopinga KK waanza kukiona

NA WAANDISHI WETU

SERIKALI ya Kenya Kwanza inaonekana kuwa na kisasi cha wazi dhidi ya maafisa wa serikali iliyoondoka ya Jubilee akiwemo Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, waliokuwa mawaziri na washirika wake.

Hatua ya serikali kubomoa sera za serikali iliyopita na matamshi ya viongozi yanaonyesha wazi kuwa inawaandama watu inaohisi ni adui zake hasa waliounga washindani wao wakuu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Wadadisi wanasema serikali ya Kenya Kwanza ilianza kisasi hicho punde baada ya kuapishwa kwa kulenga makamishna wa kikanda na kaunti na maafisa wakuu wa usalama ambao ililaumu kwa kutumiwa kisiasa na utawala wa Jubilee, na imekuwa ikizidisha kisasi dhidi ya waliokuwa maafisa wakuu serikalini na familia zao.

Rais Ruto alinukuliwa akisema alimfuta kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu, George Kinoti licha ya kusema awali alijiuzulu.

Mwezi Januari, Serikali, kupitia Wizara ya Usalama, iliwatimua makamishna wanane wa ukanda waliohudumu chini ya Jubilee. Pia iliwaadhibu makamishna wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) maarufu kama Cherera 4 waliojitenga na matokeo ya kura ya urais ambayo Dkt Ruto alitangazwa mshindi.

Kulingana na wachanganuzi, kuhakikisha makamishna wa IEBC wameondoka ofisini na kuacha tume hiyo bila kamishna baada ya aliyekuwa mwenyekiti Wafula Chebukati na wenzake Boya Molu na Abdi Guliye kustaafu, kulionyesha kiwango cha kisasi cha Kenya Kwanza dhidi ya wapinzani wake.

“Hicho kilikuwa kionjo tu, nguvu za kisasi zimeanza kuonekana sasa tena wazi kufuatia yanayofanyika kwa aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i,” asema Dkt Maria Nduku mwanaharakati.

Maafisa wa polisi walivunja nyumba ya Dkt Matiang’i ili kusaka picha za kamera za usalama”baada ya ripoti kuibuka kuwa alivamiwa na maafisa wa polisi.

DCI imemuita kuhusiana na kisa hicho huku Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) ikisema inachunguza alivyopata mali yake. Dkt Matiang’i ameagizwa kufika leo katika DCI kujibu maswali.

Kati ya masuala yanayochunguzwa ni kuchapisha taarifa ya kupotosha kinyume cha Kifungu cha 23 cha Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Kompyuta 2018. Anatarajiwa kufika DCI saa tatu unusu asubuhi la sivyo afunguliwe mashtaka kortini.

Wakili wa Dkt Matiang’i, Bw Danstan Omari anasema waziri huyo wa zamani anaandamwa kwa kuwa mshirika wa kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga na kupinga Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kisasi cha Kenya Kwanza hakijasaza vinara wa Azimio huku ikionekana kulenga biashara kubwa zinazomilikiwa na familia za Bw Kenyatta na Bw Odinga.

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametangaza wazi kuwa familia hizo zinamiliki biashara za maziwa (Kenyatta) na gesi (Odinga) na Kenya Kwanza itavunja ukiritimba wao ili kupunguzia Wakenya gharama ya bidhaa hizo anayodai iko juu kwa sababu zinadhibitiwa na familia mbili.

WAPORAJI

Ijumaa, Bw Gachagua alitangaza hatua inayolenga mawaziri zaidi wa serikali ya Uhuru kwa kusema hivi karibuni “ataanika mawaziri waliopora Sh 24 bilioni miezi mitatu ya mwisho ya utawala wa Jubilee”.

Hii itakuwa kuendeleza tangazo la Rais William Ruto lililoashiria kwamba Serikali itaandama familia za watu wenye ushawishi kwa kutolipa ushuru, lililochukuliwa kuwa alilenga familia ya Kenyatta.

Rais Ruto pia amekuwa akiwatumia maafisa wa serikali hasa wakuu wa mashirika ya umma walioteuliwa na Uhuru na kujaza nafasi hizo na washirika wake. Duru zinasema shoka la Ruto linaendelea na sasa linaelekea kwa mabalozi walioteuliwa na Uhuru.

Jana Jumatatu, Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot alisema katika mtandao kuwa Rais atafanikiwa kuangamiza makateli katika sekta zote ila huenda ikawa vigumu kuwafagia wakiritimba katika sekta za uanahabari na benki kutokana na ushawishi wao.

“Ila lazima tupate njia ya kuwamaliza (nao pia),” akaandika.

Mchanganuzi wa siasa Mutahi Ngunyi anaonya kuwa kisasi huenda kikawa hasara kwa Rais Ruto akisema anapaswa kuzingatia ajenda zake za maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Sauti za jamii ndogo zianze kusikika katika...

Maxine Wahome kupimwa akili Mathari kabla ya kujibu shtaka...

T L