• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 6:50 AM
Kwa nini Ruto aogopa Uhuru

Kwa nini Ruto aogopa Uhuru

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais Dkt William Ruto anaonekana kubadili mbinu yake ya kuwinda kura katika eneo la Mlima Kenya na sasa amenyenyekea na kuepuka kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta moja kwa moja tofauti na hapo awali.

Kauli za Naibu wa Rais Ruto za hivi majuzi kaunti za Kiambu, Nakuru na Murang’a kumtaka Rais Kenyatta kujitenga na kampeni za kinara wa ODM Raila Odinga huku akimtaja kama rafiki, zimeibua mjadala mkali miongoni mwa wadadisi wa masuala ya kisiasa na wanasiasa wa mirengo ya Azimio La Umoja na Kenya Kwanza.

Ijumaa Dkt Ruto alipokuwa katika eneo la Mutomo, Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu, ‘aliwatuma’ wakazi kumweleza Rais Kenyatta ‘asiniumize’.

“Nawatuma watu wa Mutomo muende muambie Rais Kenyatta ambaye ni jirani yenu kwamba namuomba kwa unyenyekevu. Asitumie upanga niliomsaidia kuupata kunikata miguu,” akasema Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuwa ‘upanga’ ambao Naibu Rais wa Rais alirejelea huenda alimaanisha Rais Kenyatta asitumie mamlaka yake kumpokonya ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Mwambie yule Ruto unayempangia (njama) ndiye mliombewa naye hapa Gatundu na hata hayo maombi Mama Ngina (Kenyatta) alituombea. Tafadhali muambie asiniumize. Mmwambie hata kama hataki kunisaidia aniachie huyu mtu wa kitendawili (Raila), niko tayari kupambana naye. Rais asimame kando,” akasema Dkt Ruto.

Alipokuwa katika eneobunge la Kiharu, Kaunti ya Murang’a, viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Dkt Ruto na kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, pia walimtaka Rais Kenyatta kujiondoa kwenye kampeni za urais za Bw Odinga.

“Wewe ulichaguliwa na Wakenya kuwa rais wa Jamhuri ya Kenya sio kuwa meneja wa kampeni za kitendawili (Raila),” akasema Bw Mudavadi.

Naye Dkt Ruto alisema: “Namuomba kwa heshima ndugu na rafiki yangu Rais, tafadhali wewe kaa kando achia mimi mzee wa kitendawili. Huyu nitamshinda asubuhi na mapema.”

Katika mikutano ya awali ya kampeni, Dkt Ruto amekuwa akishikilia kuwa atamshinda Bw Odinga licha ya kuungwa mkono na Rais Kenyatta na mabwanyenye wa Mlima Kenya.

Mnamo Februari 8, Dkt Ruto alipokuwa katika Kaunti ya Kakamega alisema kuwa atambwaga Bw Odinga licha ya kuungwa mkono na Rais Kenyatta.

“(Rais) anapanga mradi wake (Raila) kuwa mrithi wake. Lakini namweleza kwamba niko tayari kupambana nao. Tuko tayari kabisa.,” Dkt Ruto alisema.

Viongozi wa Kenya Kwanza wamekuwa wakidai kuwa Rais Kenyatta ana kura moja na ameishiwa na ushawishi wa kisiasa nchini likiwemo eneo la Mlima Kenya.

Wandani wa Bw Odinga wanasema kuwa hatua ya Naibu wa Rais kubadili kauli na kumsihi Rais Kenyatta kujitenga na siasa ni ishara kwamba ameanza kutambua kwamba Rais Kenyatta angali na ushawishi mkubwa.

Mwakilishi wa Wanawake wa Uasin Gishu Gladys Shollei jana Jumatatu alionekana kukiri kuwa hatua ya Rais Kenyatta kuingilia kampeni za Bw Odinga huenda ikawa pigo kwa Dkt Ruto.

“Raila hawanii urais bali anayewania ni Rais Kenyatta. Rais amesimama katikati ya Raila na Naibu wa Rais kwa lengo la kumtishia Dkt Ruto,” akadai Bi Shollei.

Mbunge wa Kimilili Didmus Wekesa Barasa anasema kuwa hatua ya Dkt Ruto kumsihi Rais Kenyatta kujitenga na kampeni za Bw Odinga si ithibati kwamba anamuogopa.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto hata hivyo, anakiri Rais Kenyatta amesaidia kuinua kampeni za Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Ida aahidi kuinua maisha ya wanawake vijijini Raila akiwa...

Timu za voliboli ya ufukweni zawasili nchini Ghana kusaka...

T L