• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Maeneo bunge yasiyo na idadi tosha ya watu kumezwa

Maeneo bunge yasiyo na idadi tosha ya watu kumezwa

NA MERCY KOSKEI

UFICHUZI kwamba, karibu maeneo bunge 40 nchini yatafutiliwa mbali kwa sababu hayajatimiza idadi ya watu wanaohitajika kulingana na sheria, umeibua wasiwasi miongoni mwa wabunge wanaoyawakilisha.

Hayo yalifichuka Jumatano, wakati wa warsha kuhusu mageuzi katika mfumo wa uchaguzi iliyofanyika katika mkahawa mmoja mjini Nakuru.

Kulingana na sheria, kila mojawapo ya maeneo bunge 290 linapaswa kuwa na angalau watu 164,137, idadi ambayo imekadiriwa kutokana na jumla ya idadi ya watu 47.6 milioni nchini kulingana na sensa ya 2019.

Kwa hivyo, kwa misingi hiyo, miongoni mwa maeneo bunge ambayo huenda yakafutuliwa mbali wakati wa shughuli ya uwekaji mipaka upya mwaka 2024 ni Lamu Mashariki inayowakilishwa na Ruweida Obo na yenye watu 22,258, Mwatate (Peter Mbogho, 81,659), Kuria Mashariki (Marwa Kitayama, 96,872), Mlima Elgon (Fred Kapondi, 78,873), Voi (Khamis Chome,111,831) na Tiaty (William Kamket,73,424).

Mengine ni pamoja na Laikipia Kaskazini yenye watu 36,184, na inayowakilishwa na Sarah Korere, Kathiani (Robert Mbui, 111,890), Keiyo Kaskazini (Adam Kipsanai, 99,176), Eldas (Adan Keynan, (88,509), Kangundo (Fabian Muli, 97,917) na Budalang’i (Raphael Wanjala 85,977).

Pia kuna Tiaty (73,424), Keiyo Kaskazini (99,176), Marakwet Mashariki (97,041), Loima (107,795), Kangema(80,447), Tetu (80,453), Mathioya (92,814), Mukurwe-in (89,137), Kang’undo (97,917), Mwingi Mashariki (85,139), na Lafey (83,457).

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inatarajiwa kuanza shughuli ya kuweka upya mipaka ya maeneo ya uwakilishi mnamo Machi 2024, kwa ajili ya kutumika katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Kulingana na Katiba, tume hiyo itabadilisha majina na mipaka ya maeneo bunge ndani ya muda usiopungua miaka minane au kuzidi miaka 12.

Mabadiliko ya mwisho ya mipaka ya maeneo bunge yalifanyika mnamo Machi 2012. Hii ina maana kuwa, shughuli hiyo inapasa kuanzia Machi 2024 na kukamilika angalau miezi 12 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) inataka mipango ya kufutiliwa mbali kwa maeneo bunge yasiyotimiza hitaji la kisheria kuhusu idadi ya watu, isitishwe.

Badala yake, baadhi ya wanachama wa kamati hiyo wanataka mchakato wa uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC uharakishwe ili kusaidia kughulikia suala hilo. Wanataka suala hilo la kukinga maeneo bunge hayo lishughulikiwe ndani ya miezi mitano ijayo. Kulingana na mbunge wa Gatanga Edward Muriu, kufutiliwa mbali kwa maeneo bunge 40 kutasababisha mzozo wa kikatiba na kiuchaguzi nchini.

“Maeneo bunge hayo yanafaa kukingwa kwa hali zote dhidi ya kufutuliwa mbali ndani ya miezi mitano ijayo ili tuzuie mizozo isiyo na maana. Hii ni licha ya kwamba maeneo bunge hayajaafikia idadi hitajika ya watu,” akasema mwanachama huyo wa JLAC.

“Aidha, tunataka Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo inayoongozwa na Kalonzo Musyoka na Kimani Ichung’wa kuingilia kati na kuzuia kufutiliwa mbali kwa maeneo bunge hayo. Naomba kwamba, huku mazungumzo ya Bomas yakiendelea, jopo la kuteua makamishna wa IEBC liruhusiwe kuendelea na majukumu yake, liteue makamishna ili waanze shughuli ya kubadilisha mipaka,” Bw Muriu akaongeza.

Bw Musyoka ambaye aliwakilisha muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya katika warsha hiyo jijini Nakuru pia anapendekeza kuwa maeneo bunge hayo 40 yadumishwe.

  • Tags

You can share this post!

Demu aamua wanaommezea mate wafanye ‘interview’

Salasya: Natafuta mwanamke Mzungu wa kuoa

T L