• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:49 PM
Magavana msalabani manaibu wao wakisuka njama ya kuwazika kisiasa

Magavana msalabani manaibu wao wakisuka njama ya kuwazika kisiasa

Miongoni mwa magavana hao ni Kawira Mwangaza (Meru) na Amos Nyaribo (Nyamira) ambao madiwani wametishia kuwatimua mamlakani.

Dkt Eric Mutai (Kericho), Mutula Kilonzo Junior (Makueni), James Orengo (Siaya), Wavinya Ndeti (Machakos) na Fernandes Barasa (Kakamega) nao wamelalamikia vikali uhusiano wao na manaibu wao, madiwani au maafisa wakuu wa serikali zao.Katika Kaunti ya Meru, zaidi ya madiwani 60 kati ya 69 katika bunge la kaunti hiyo wametia saini kuunga mkono hoja ya kumng’oa mamlakani Bi Mwangaza kama gavana.

Madiwani hao wanamlaumu Bi Mwangaza kwa kuendesha masuala ya kaunti bila kuwashirikisha ifaavyo. Wengine wanamlaumu kwa kuigeuza kaunti kuwa kama “mali ya familia yake.” Madiwani hao wamepanga kuwasilisha hoja hiyo mwezi ujao.

Mnamo Jumanne, duru ziliiambia Taifa Leo kuwa, juhudi za kuwahusisha vigogo wa kisiasa kutoka ukanda wa Mlima Kenya kama Naibu Rais Rigathi Gachagua, mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Mithika Linturi (Kilimo) na aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo, Kiraitu Murungi, kusuluhisha mzozo huo zimegonga mwamba.

Hili litakuwa jaribio la pili madiwani hao kutishia kumwondoa mamlakani Bi Mwangaza, baada yake kuokolewa na Seneti Desemba 2022.

Katika Kaunti ya Nyamira, madiwani jana Jumanne waliorodhesha sababu zaidi ya 10 za kumwondoa afisini Bw Nyaribo.

Baadhi ya sababu hizo ni kwamba, gavana huyo amekuwa akikiuka Katiba na kuwaajiri wafanyakazi bila kufuata taratibu zifaazo za kisheria.

Lawama nyingine ni kupuuza maagizo ya mahakama, kutotuma pesa za makato ya wafanyakazi wa umma na kuajiri kazi jamaa wake wa karibu.

Sababu hizo ziliwekwa bayana wakati hoja ya kung’atuliwa kwake iliwasilishwa bungeni na diwani Josiah Mang’era (Esise).

Katika Kaunti ya Makueni, Gavana Mutula Kilonzo Junior, jana Jumanne alifanya kikao cha ghafla na kuwazomea vikali maafisa wa ngazi za juu katika kaunti hiyo, ambao wamekuwa wakifichua “mapungufu” ya utawala wake katika mitandao ya kijamii.

Ripoti zinaeleza kuwa, Bw Kilonzo ameanza kuhofishwa na malalamishi ambayo yamekuwa yakitolewa na wakazi kuhusu kudorora kwa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali za kaunti hiyo.

Katika hali inayoonyesha mivutano ya kichinichini iliyoko katika serikali hiyo, maafisa wengi wa ngazi za juu wamekuwa wakiweka stakabadhi zinazoeleza mivutano iliyopo kwenye mitandao ya kijamii.

Hali pia si shwari katika Kaunti ya Siaya, baada ya kuibuka kuwa, serikali ya Bw Orengo inakabiliwa na sakata kubwa ya utoaji ajira, hali inayotishia kuipotezea mamilioni ya pesa.Pia, Bw Orengo na Naibu Gavana William Oduol bado hawajazika tofauti zao.

Bw Oduol aliokolewa na Seneti mnamo Juni baada ya madiwani kupiga kura ya kumng’oa mamlakani.

Katika Kaunti ya Kericho, mvutano baina ya Dkt Mutai na Naibu Gavana Fred Kirui ulianza miezi michache tu baada yao kuanza kuhudumu.

Dkt Mutai amekuwa akimlaumu Bw Kirui kwa kumdharau, huku Bw Kirui akimlaumu Dkt Mutai kwa kutozingatia mkataba wa kisiasa waliotia saini wakati wa kampeni. Bw Kirui amekuwa akidai kwamba, Dkt Mutai amewasahau “watu wake”.

Baadhi ya viongozi ambao wameingilia mzozo huo ni Bw Gachagua, aliyewaonya wawili hao dhidi ya “kuipaka tope” serikali ya Kenya Kwanza.

Katika Kaunti ya Machakos, Bi Ndeti amekuwa akivutana na Naibu Gavana Francis Mwangangi. Bi Ndeti alimpokonya gari rasmi huku tofauti zao zikigawanya madiwani.

Katika Kaunti ya Kakamega, kulizuka mvutano baina ya Bw Barasa na Naibu Gavana Ayub Savula huku mbunge huyo wa zamani wa Lugari akidai ni gavana-mwenza, wala si naibu wa Bw Barasa. Wawili hao walitangaza kuzika tofauti zao baada ya kulaumiana hadharani.

  • Tags

You can share this post!

Kamati ya mdahalo wa kitaifa kutumia Sh106m kutafuta namna...

Mke alia akidai mume hampi haki yake chumbani

T L