• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Masuala yanayomfanya Mudavadi ‘kuchukia’ Raila

Masuala yanayomfanya Mudavadi ‘kuchukia’ Raila

CECIL ODONGO na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kuonekana kukerwa hadharani na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusiana na kinyang’anyiro cha urais 2022, imeibua maswali tele.

Wadadisi wanasema kuwa, tofauti baina ya Bw Mudavadi na Bw Odinga ni za kisiasa.Wakili na Mtaalamu wa Masuala ya Utawala, Javas Bigambo, anasema Bw Mudavadi amekerwa na hatua ya Bw Odinga kuonekana kutomthamini.“Katika uchaguzi wa 2017, Bw Mudavadi alikuwa meneja wa kampeni za Bw Odinga.

Mudavadi hakupewa wadhifa wowote. Mudavadi anajua wazi kwamba hatakuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga na akiamua kumuunga itabidi awe meneja wa kampeni tena,” anasema Bw Bigambo.Bw Bigambo hata hivyo anasema Bw Mudavadi itabidi afanye kazi na Bw Odinga ili kujiongezea nafasi ya kuwa serikalini katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kumekuwa na madai kuwa Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiwashinikiza vigogo wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA); Bw Mudavadi, Bw Kalonzo Musyoka (Wiper), Bw Gideon Moi (Kanu), Bw Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Bw Cyrus Jirongo (UDP) wamuunge mkono Bw Odinga.Bw Mudavadi amekuwa akifoka mara kwa mara katika mikutano ya kisiasa akisema viongozi hawafai kulazimishwa kuunga mkono mwaniaji fulani wa urais.

Kauli hiyo ya kiongozi wa ANC inaonekana kumrejelea Rais Kenyatta ambaye amekuwa akikutana faraghani na viongozi wa OKA pamoja na Bw Odinga kujadili siasa za urithi 2022.Katika Kongamano la Wiper Alhamisi, Bw Mudavadi alionekana kumsalimia Bw Odinga shingo upande – hali ambayo ilizua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii kuhusu kiini cha tofauti zao.

Baada ya hafla hiyo, Bw Musalia aliweka picha za viongozi kadhaa waliohudhuria katika mitandao yake ya kijamii lakini akakosa kuweka ya Bw Odinga.Chama cha ANC pia hakikuweka picha za Bw Odinga katika mitandao yake ya kijamii.Licha ya kuwa wanasiasa hao wawili walishirikiana kisiasa mnamo 2007 na 2017, Bw Mudavadi mara hii amekuwa akionyesha hadharani hasira zake dhidi ya Bw Odinga huku akishikilia kuwa lazima jina lake liwe debeni.

Baadhi ya wadadisi wanasema kuwa, iwapo Bw Mudavadi atakuwa debeni 2022 atagawa kura za Magharibi na kunyima Bw Odinga ushindi.Lakini Bw Bigambo anasema kwamba, ushawishi wa Bw Odinga katika eneo la Magharibi ni mkubwa hivyo Bw Mudavadi atakuwa na kibarua kikubwa kuhakikisha kuwa anaweka kibindoni angalau asilimia 70 ya kura za Mulembe.

Mbunge wa Shinyalu Justus Kizito anasema Bw Mudavadi anaonekana kukerwa na hatua ya Bw Odinga kukataa kumuunga mkono 2022.“Tunafahamu kuhusu chuki hizo na sisi kama ODM hatuna haja na kumfuatilia ndiyo maana tunazungumza na wapigakura wa Magharibi moja kwa moja kupitia kampeni zetu.

Hata kama ni kumsaidia, utamfaa vipi mtu ambaye hana uungwaji mkono hata katika ngome yake na washirika wake wanakesha kwa Ruto usiku na mchana wako naye,” akasema Kizito.“Vinara wengine wa OKA wameonyesha hawana tatizo na kufanya kazi na Bw Odinga isipokuwa yeye.

Tushajua lengo lake ni kugawa kura za Magharibi jinsi alivyofanya 2013 kisha aunde serikali na Dkt Ruto lakini hatutakubali kuelekea njia hiyo,” akaongeza.Mtaalamu wa Masuala ya Kisiasa Martin Andati anadai kuwa uhasama kati ya viongozi hao wawili wakuu ni kuhusu rasilimali zilizowekezwa katika kampeni za muungano wa Nasa kuelekea kura ya 2017.

“Ukitazama vizuri Mudavadi ashakata kauli ya kuenda hadi debeni kinyume na Kalonzo, Wetangula, Moi na Jironga ambao huenda hapo mbeleni wakashawishiwa kumuunga Raila.“Tatizo kati ya Mudavadi na Bw Odinga ni kuhusu pesa zilizotolewa za kufanyia Nasa kampeni 2017 na anahisi kusalitiwa kwa sababu alikuwa na mchango mkubwa sana kifedha kwenye kampeni hizo,” anadai Bw Andati ambaye alihudumu katika sekretariati ya Nasa.

Anadai kuwa Bw Mudavadi hajarejeshewa fedha alizotumia katika kampeni za NASA hata baada ya Bw Odinga kufanya handisheki na Rais Kenyatta.Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha United States International University Africa (USIU) Profesa Macharia Munene naye anasema tofauti kati ya Mabw Mudavadi na Odinga ni za kisiasa wala si za kibinafsi.

Anashikilia kuwa iwapo kinara huyo wa ANC hatasimama 2022, basi huo utakuwa mwisho wake wa kisiasa.“Wafuasi wa Raila na Musalia, wote wameshikilia msimamo mkali kuwa lazima viongozi hao wawe debeni. Tatizo ni kuwa Musalia haamini Raila tena na analenga kujenga himaya yake hata asiposhinda.

Kwa kuwa alijikwaa 2002 na 2013, uchaguzi wa 2022 utampa uhai zaidi kisiasa kuliko Raila ambaye pia umri unasonga,” akasema Profesa Munene.“Ukimwangalia Musalia na umpime na vinara wengine wa OKA, anaonekana kuwa kifua mbele kutokana na ukomavu wake na anakubalika miongoni mwa jamii mbalimbali nchini.

Si kama Kalonzo ambaye hubadilisha msimamo wake wa kisiasa mara kwa mara na hatabiriki,” akaongeza.Huku wajumbe wa ODM wakitarajiwa kuwa na Kongamano Kuu la Wajumbe (NDC) mnamo Disemba 9 la kumuidhinisha kuwania Urais 2022, wengi wanasubiri kuona iwapo Bw Mudavadi atahudhuria na kile atakachozungumzia kuhusu waziri huyo mkuu wa zamani

You can share this post!

Ni kisasi tu wikendi hii!

Cotu yamtaka Matiang’i asikize kilio cha polisi

T L