• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Mbadi sasa adai vijana waliomshambulia Raila walikuwa na mafunzo ya ‘kijeshi’

Mbadi sasa adai vijana waliomshambulia Raila walikuwa na mafunzo ya ‘kijeshi’

NA CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa ODM John Mbadi sasa anadai kuwa vijana walioshambulia helikopta ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika kaunti ya Uasin Gishu, Ijumaa wiki jana huenda walikuwa wamepewa mafunzo maalum.

Akiongea afisini mwake katika majengo ya bunge, Nairobi, Jumatatu, Apili 4, 2022 mbunge huyo alidai kuwa vijana hao walidhihirisha ujuzi wa kijeshi, ishara kwamba walipanga kumshambulia Bw Odinga.

“Baada ya kutizama kwa makini video kuhusu tukio hilo la kuogofya nimeng’amua jinsi walivyojipanga, walivyotekeleza mashambulio, umakinifu, mawasiliano kati yao, walivyokaidi maafisa wa polisi na nikagundua kuwa hawa hawakuwa vijana wa kawaida. Kuna uwezekano mkubwa kwamba walikuwa wamepokea mafunzo fulani ya kivita,” Bw Mbadi akawaambia wanahabari.

Mbunge huyo wa Suba Kusini, ambaye ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa, alitaka serikali kuchunguza uwezekano kwamba huenda kuna watu wanaotoa mafunzo ya “kijeshi” kwa vijana kwa lengo la kuwatumia kwa manufaa yao ya kisiasa.

“Kwa hivyo, polisi wasichunguze tu uwezekano wa kuwepo kwa mawasiliano na upitishwaji wa pesa kwa vijana hao na wanasiasa waliokamatwa, polisi wachunguze mienendo ya vijana hao kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita,” Bw Mbadi akasema.

Kiongozi huyo wa ODM alielekeza kidole cha lawama kwa viongozi wa UDA katika kaunti ya Uasin Gishu akisema ni wao ndio walipanga mashambulio dhidi ya Bw Odinga.

“Hawa watu walifanya hivi baada ya kung’amua kuwa watashindwa katika kinyang’anyiro cha Urais Agosti 9. Lakini ningependa kuwaonya kwamba wakome kuwatumia vijana kwa njia mbaya jinsi hiyo,” Bw Mbadi akasema.

Mnamo Jumapili Mbunge wa Soy Caleb Kositany na mwenzake wa Kapseret Oscar Sudi pamoja na Spika wa Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu David Kiplagat waliandikisha taarifa kwa afisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Nakuru kuhusiana na tukio hilo.

Bw Odinga na viongozi alioandamana nao walishambuliwa Ijumaa baada ya kutoka katika boma la marehemu Mzee Jackson Kibor ambako walikuwa wameenda kufariji familia hiyo.

Viongozi kadha, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta wamelaani kitendo hicho na kusema hakifai kutokea wakati kama huu ambapo taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu.

  • Tags

You can share this post!

Man City vs Atletico patachimbika UEFA

Serikali ya Kenya yatoa Sh34 bilioni za kukabiliana na kero...

T L