• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Mikakati ya UDA kuzuia kuhepwa

Mikakati ya UDA kuzuia kuhepwa

NA SIAGO CECE

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA), kimeanza kujizatiti kurudishia wafuasi wake imani baada ya kutorokwa na baadhi ya wanasiasa waliodai hakuna haki chamani.

Chama hicho sasa kimefahamisha wafuasi wake kwamba hakuna mwanasiasa ambaye atapewa tikiti ya moja kwa moja, isipokuwa kama kutakuwa na mmoja pekee atakayewasilisha ombi la kutaka kuwania kiti hicho.

Katika mkutano wa kwanza wa wajumbe wa UDA kutoka Kaunti ya Kwale, maafisa wa chama walitoa wito kwa wanasiasa wanaotaka kuwania viti kupitia chama hicho watume maombi yao bila wasiwasi.

Mratibu wa chama hicho wa Kwale Richard Itambo, alisema uteuzi unatarajiwa kufanyika kati ya Aprili 9 na Aprili 16.

Bw Itambo alisema ingawa kuna kura za maoni zilizokuwa zimefanywa awali kutafuta wanasiasa maarufu, huenda ikawa matokeo hayo yatakuwa yamepitwa na wakati kufikia Agosti.

Alisema chama bado hakijaamua nani apate tikiti ya moja kwa moja kwa kuwa waombaji wengine wengi bado wanaleta maombi yao ya kujiunga na chama.

“Tukishapokea maombi ndipo tutajua nani anapewa tiketi ya moja kwa moja na ni wangapi wataenda kwa kura ya mchujo,” akasema.

Baadhi ya wanasiasa waliokuwa wanataka kuwania tikiti za uchaguzi ujao kuwania ugavana Pwani walikihama wakidai kulikuwa na uwezekano wapinzani wao kupewa tikiti za moja kwa moja.

Hii ni baada ya Dkt William Ruto anayeongoza UDA kuonyesha ukaribu wake na wanasiasa kama vile Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani na aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Bw Omar Hassan, wanaotaka kuwania ugavana katika kaunti zao.

Wanasiasa kadha wanaotaka viti vingine pia walihama, na kujiunga na vyama vingine.

Katika mkutano huo wa wajumbe uliofanywa mwishoni mwa wiki ukiongozwa na mwakilishi kutoka Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya UDA, Bw Chacha Matiko, ilibainika kuwa mojawapo ya masuala makuu yaliyoibuka ni kutafuta hakikisho la wanachama kwamba yule atakayeshindwa katika mchujo ataunga mkono mshindi wa tikiti.

Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, alisema ni muhimu chama hicho kiwe na viti vingi iwezekanavyo wakati wa Uchaguzi Mkuu.

“Lazima tujenge chama chetu na kuwasilisha viti zaidi kwa Naibu Rais wetu na chama,” akasema, huku akitoa wito wa umoja kati ya wanaowania nafasi hiyo.

Bi Achani, Bw Mwashetani, Mbunge wa Kinango, Bw Benjamin Tayari, na mwenzake wa Msambweni, Bw Feisal Bader ni miongoni mwa wanaotarajiwa kupata uteuzi wa moja kwa moja.

Bw Tayari alisema suala la tikiti ya moja kwa moja litategemea orodha ya mwisho ya usajili, kwani wawaniaji zaidi walikuwa wakijiunga na chama hicho kutaka kuwania viti tofauti.

“Tunakaribisha kila mtu kujiunga na chama chetu kwa sababu tuko na usawa,” Bw Tayari alisema.

Haya yanajiri huku chama hicho kikipanga mkutano mkubwa kesho Jumanne eneo la Lungalunga kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani.

Kinara mwenza wa Muungano wa Kenya Kwanza, Bw Moses Wetang’ula anatarajiwa kuongoza mkutano huo.

Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, bado alikuwa katika ziara ya ng’ambo alikoandamana na Dkt Ruto pamoja na viongozi wengine wa UDA.

Ziara hizo zilinuiwa kuwafikisha katika mataifa ya Amerika na Uingereza.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Mzozo Ukraine umeibua upya Vita Baridi...

Kaunti zaidi ya 15 zakosa rekodi za ‘utajiri’ wake

T L