• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Mikakati yake Uhuru kuzima Ruto Mllimani

Mikakati yake Uhuru kuzima Ruto Mllimani

NA MWANGI MUIRURI

KIBARUA kigumu kinamngoja Rais Uhuru Kenyatta katika jitihada zake za kukomesha umaarufu wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya na badala yake kuinua ule wa Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Dkt Ruto amekuwa akijipigia debe eneo hilo kwa zaidi ya miaka minne sasa, na ni dhahiri kuwa ana uungwaji mkono mkubwa ikilinganishwa na Bw Odinga, ambaye anapendelewa na Rais Kenyatta kuwa mrithi wake.

Katika juhudi za kumaliza umaarufu wa naibu wake, Rais Kenyatta na washirika wake wamepanga mikakati wanayosema itazima umaarufu wa Dkt Ruto.

Waziri wa Kilimo, Peter Munya aliambia Taifa Leo kuwa wamepanga mikakati ambayo karibuni itampa umaarufu mkubwa Bw Odinga.

Mikakati hiyo, Bw Munya asema, ni pamoja na kuharakisha kukamilishwa kwa miradi inayoendelea eneo hilo na rais kufanya ziara nyingi eneo hilo, kinyume na sasa ambapo ni nadra kwake kufanya vikao na wakazi.

HISIA ZA KUPUUZWA Baadhi ya wadadisi wanasema umaarufu wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya umechangiwa na hisia kuwa Rais Kenyatta amewapuuza waliompigia kura kwa wingi 2013 na 2017 hasa kiuchumi.

“Tutapunguza bei ya uzalishaji katika sekta ya kilimo ili pato kwa wakulima lipande, miradi inayoendelea itakamilishwa, wafanyabiashara wasaidiwe na wanaodai serikali

walipwe. Tuko na imani kwamba tutafanikiwa kushawishi wapiga kura watuunge mkono,” akasema Bw Munya.

Lakini wengine wanasema Rais Kenyatta na washirika wake watakuwa na kibarua kigumu kubadilisha hali.

“Shida tuliyo nayo ni kwamba wengi wa wapiga kura wa Mlima Kenya wanamchukulia Uhuru kama aliyewapuuza. Itabidi awaeleze sababu za kilimo cha kahawa na chai kukosa kuboreshwa, kilichofanya wafanyibiashara wa Nyamakima kuharibiwa biashara zao miongoni mwa matatizo mengine wanayopitia wakazi,” asema Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua.

“Hisia za wengi mashinani ni kuwa Uhuru ‘anawachukia’ watu wa Mlima Kenya. Pia wanamlaumu kwa mgawanyiko wa jamii za Mlima Kenya,” asema Bw Gachagua.

KUTULIZA HASIRA Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata anasema mambo ambayo washirika wa rais wanapangia Mlima Kenya yangemsaidia rais kusikizwa na wakazi yangefanywa mapema.

“Shida ni kwamba wamechelewa kwa kuwa wangefanya hayo kitambo. Kuna washauri wa rais wenye kiburi ambao ndio wamefanya apoteze sauti Mlima Kenya,” asema Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri.

Lakini Kiongozi wa Wengi Bungeni, Amos Kimunya anasema kuwa rais amejipanga vizuri na kabla ya Aprili hali itakuwa tofauti na sasa.

“Rais ametuhakikishia kuwa pendekezo lake Mlimani ni Bw Odinga ili atuhakikishie amani na ustawi. Rais mwenyewe ndiye kinara wa kampeni za Bw Odinga,” asema

Mbunge wa Gatanga, Nduati Ngugi.

Msimamo huo unatiliwa mkazo na Waziri wa Uchukuzi, James Macharia ambaye aliambia Taifa Leo kwamba rais amewaambia mawaziri wanaotoka Mlima Kenya wampigie debe Bw Odinga.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth anasema Rais Kenyatta ana jibu kuhusu urithi wa msemaji wa kijamii na pia wa urais.

WAKAZI KUJUTA WAKIKAIDI RAIS

Bw Kenneth, ambaye ndiye anaonekana kupendelewa na rais awe msemaji wa jamii za Mlima Kenya na ateuliwe kuwa naibu wa rais katika serikali ya Bw Odinga, anashikilia kuwa kunahitajika tu mikutano mikubwa ambapo rais na wafuasi wake watajitetea.

“Rais ana ujanja wa kipekee wa kisiasa. Ni mweledi wa hotuba na anajua anachofanya ni kwa manufaa ya ngome yake na uwiano wa kitaifa,” asema Bw Kenneth.

Mbunge Mwakilishi Mwanamke wa Murang’a, Sabina Chege anasema ikiwa Mlima Kenya utakaidi Rais Kenyatta utajuta baadaye.

Mshirikishi wa Wakfu wa Mlima Kenya, Peter Munga aliambia Taifa Leo kwamba Rais Kenyatta atastaafu akiwa mmoja wa mashujaa wa kijamii.

“Uhuru amepanua uchumi, ameleta uthabiti wa kitaifa na amani ambazo zinasaidia wafanyabiashara wa Mlima Kenya kukubalika kuwekeza katika kona zote za nchi. Ni katika msingi huo ambapo mabwanyenye wa kijamii pamoja na wanasiasa watiifu kwa rais tumeungana kusema kwamba maslahi yetu yanaweza tu kutekelezwa na kutimizwa na Bw Odinga,” akasema Bw Munga.

  • Tags

You can share this post!

Msitu wa Arsenal kunyanyua hadhi ya kijiji cha Shingwaya

Kiwanda cha betri kufungwa baada ya marufuku ya vyuma

T L