• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 6:55 PM
Msaidizi wa Murkomen pia ahojiwa kuhusu shambulio

Msaidizi wa Murkomen pia ahojiwa kuhusu shambulio

NA FRED KIBOR

POLISI katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, wamemhoji msaidizi wa Seneta Kipchumba Murkomen kuhusiana na kuzomwa na kushambuliwa kwa mawe kwa msafara wa mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga mjini Iten mnamo Ijumaa wiki jana.

Taifa Leo imebaini kuwa wanasiasa zaidi wa kaunti hiyo wameitwa kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo, ingawa wapelelezi wamekataa kutaja majina yao wakisema uchunguzi unaendelea.

Bw Adams Kipsanai, mwaniaji wa kiti cha Keiyo North kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), alisema kwamba alihojiwa na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) mjini Itenkwa zaidi ya saa tatu mnamo Jumatatu jioni, kuhusiana na madai ya kupanga ghasia zilizomfanya Bw Odinga kukatiza ziara yake katika eneo hilo.

“Nilishangaa nilipoitwa kwa sababu sikuhusika na kilichotendeka Ijumaa,” aliambia Taifa Leo.

Kamanda wa polisi kaunti ya Elgeyo Marakwet, Bw Patrick Lumumba, alisema kwamba mwanasiasa huyo aliitwa kuandikisha taarifa kuhusu tukio la Ijumaa.

“Sitazungumzia suala hilo kwa sababu uchunguzi unaendelea na wale ambao walihusika hatimaye watakabiliwa na sheria,” alisema.

Kulingana na DCI, uchunguzi wa mwanzo Jumamosi, vijana waliorushia mawe msafara wa Bw Odinga, ikiwemo helikopta yake, walichochewa kufanya hivyo.

Bw Odinga alilazimika kukatiza mkutano wake Iten baada ya vijana kuanza kumzoma huku baadhi yao wakirushia mawe magari yaliyokuwa kwenye msafara wake.

Gavana wa Elgeyo Marakwet, Bw Alex Tolgos, alikuwa amemtambulisha Bw Odinga kwa umati kando ya barabara lakini wakazi walianza kuimba wakisifu UDA.

Akithibitisha kuhojiwa kwake, Bw Kipsanai alisema wapelelezi walikagua simu yake wakati wa kikao hicho cha saa tatu.

“Wachunguzi waliniitisha simu yangu na kuangalia WhatsApp, rekodi za mawasiliano na hata za kutuma pesa. Waliniuliza kwa nini mmoja wa wafuasi wangu alikuwa akizunguka akiwa na pesa nyingi siku ambayo Bw Odinga alishambuliwa, kitu ambacho sikuwa na habari,” alisema.

Alitaja kuitwa kwake na kuhojiwa kama vitisho vya kisiasa akisema haungi aina yoyote ya ghasia za kisiasa.

“Ninahimiza wapinzani wangu kwenda kwa wapigakura moja kwa moja na kuomba kura badala ya kujihusisha na vitendo kama hivi. Niliambia polisi ninachojua kuhusu ghasia hizo kabla ya kuniachilia lakini hawafai kuchukua hatua inayoweza kuvuruga amani,” alisema Bw Kipsanai.

Tayari mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na mwenzake wa Soy, Bw Caleb Kositany na spika wa bunge la kaunti ya Uasin Gishu, Bw David Kiplagat wamehojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Mnamo Jumatatu, polisi waliruhusiwa kuendelea kuwazuilia watu 17 waliokamatwa kuhusiana na kisa hicho.

  • Tags

You can share this post!

Rais aomboleza mbunge wa zamani

Bunge lajadili kwa uzito changamoto ya uhaba wa mafuta

T L