• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 11:13 AM
Msukosuko wachemka katika Azimio

Msukosuko wachemka katika Azimio

ONYANGO K’ONYANGO,CHARLES WASONGA Na BENSON MATHEKA

MGOGORO ulioibuka ndani ya Azimio la Umoja-One Kenya kuhusu ugavi wa nafasi kwenye kamati za seneti huenda ukaathiri uthabiti katika muungano huo unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga. 

Iwapo Bw Odinga na vinara wenza wa Azimio hawatachukua hatua za haraka kuuzima, huenda ukalipuka na kuvunja muungano huo mapema.

Mzozo huo ulilipuka baada ya Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni kuusuta uongozi wa Azimio katika bunge hilo kwa kugawa nafasi hizo kwa mapendeleo.

Uongozi huo unajumuisha Kiongozi wa Wachache, Stewart Madzayo (Seneta wa Kilifi), naibu wake Enoch Wambua (Seneta wa Kitui), kiranja wa wachache Fatuma Dullo na naibu wake Ledama Ole Kina.

Bw Omogeni aliwataja wanne hao kama “walafi” kwa kutomteua mwanachama wa kamati yoyote ya bunge hilo “ilhali eneo la Gusii limesimama na Bw Odinga kwa miaka mingi.”

“Ikiwa umepewa nafasi ya uongozi, unafaa kuwa muungwana, unafaa kuwahudumia watu wote bila mapendeleao. Lakini katika upande wetu wa walio wachache, viongozi wetu wamejipatia nafasi katika kamati zote za muhula mmoja, Aibu kwetu! Aibu kwetu!” akafoka Seneta Omogeni.

Kulingana na seneta huyo, Azimio ilibagua eneo la Gusii wakati wa uteuzi wa uongozi wake katika Bunge la Kitaifa na Seneti ilhali lilimpa Bw Odinga kura nyingi zaidi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Hakuna anayefaa kuchukuliwa kama spesheli katika mchango wa kumvutia kura kiongozi wa chama chetu Raila Odinga. Katika kaunti yetu ya Nyamira tulimpa Raila kura 129,000 ilhali kutoka Isiolo alipata kura 26,000 pekee. Lakini sasa shukrani mnayotoa kwa jamii ya Abagusi ni kuwanyima nafasi katika kamati za seneti,” akasema Bw Omogeni.

Malalamishi ya Seneta Omogeni yanajiri wakati ambapo anavutana na Seneta wa Siaya Oburu Oginga kuhusu nafasi ya kuwa mwakilishi wa ODM katika Kamati ya Huduma za Bunge (PSC).

Seneta huyo wa Nyamira anashinikiza kuwa yeye ndiye anafaa kupewa nafasi hiyo kwa misingi ya mchango wake katika chama hicho.Naye Dkt Oginga, ambaye ni kakake Bw Odinga, anamezea mate nafasi hiyo yenye hadhi na ushawishi mkubwa.

PSC ndio husimamia masuala ya uajiri na maslahi ya wabunge na wafanyakazi wote katika asasi ya bunge.Mzozo huu unaakisi ule ambao ulitokea katika Bunge la Kitaifa mwezi jana kuhusu uteuzi wa uongozi wa mrengo wa Azimio katika bunge hilo.

Hii ni baada ya Mbunge Maalum John Mbadi kupinga uteuzi wa Mbunge wa Ugunja James Opiyo Wandayi kuwa kiongozi wa wachache.Hata hivyo, suala hilo lilitatuliwa baada ya Bw Mbadi kuahidiwa wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC).

Nafasi hiyo pia inamezewa mate na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ambaye pia anahisi anapasa kutuzwa kutokana na machango wake katika kampeni za urais za Bw Odinga.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, ni Bw Odinga anayefaa kuzima mgogoro katika Azimio, ukiwemo unaohusu nafasi za kamati katika seneti.

“Almradi kaka yake ametajwa kwa kutengewa nafasi zaidi katika kamati huku wengine wakikosa, kuna hatari katika Azimio. Muungano huo unaweza kulipuka na kusambaratika mapema ikizingatiwa upande wa serikali unawania kuongeza idadi ya wanachama wake katika Seneti na Bunge la Kitaifa,” akasema Dkt Gichuki.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ateua mpelelezi mwenye tajriba kurithi Kinoti DCI

Rigathi ataka Raila, Kalonzo waipe serikali ya Kenya Kwanza...

T L