• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Mwangaza asubiri kikao cha bunge la kaunti kupata mwanga kuhusu masaibu yake

Mwangaza asubiri kikao cha bunge la kaunti kupata mwanga kuhusu masaibu yake

NA DAVID MUCHUI

HUKU mikakati ya kumwondoa mamlakani Gavana Kawira Mwangaza wa Meru ikikaribia kutimia, kila upande unajikakamua kuhakikisha msimamo wake unadumishwa.

Gavana huyo anatarajiwa kujitetea Jumatano asubuhi katika Bunge la Kaunti dhidi ya madai yanayomkabili. Bunge lilo kisha litajadili na kupigia kura hoja ya kumng’oa mamlakani nyakati za adhuhuri.

Hilo linajiri baada ya bunge hilo kuandaa vikao vya umma Jumatatu, ambapo wakazi kutoka sehemu tofauti za kaunti walitoa maoni yao kuhusu hatua ya kumng’oa mamlakani kiongozi huyo.

Gavana Mwangaza anakabiliwa na mashtaka saba ya ukiukaji mkubwa wa Katiba na matumizi mabaya ya mamlaka.

Katika patashika hiyo, Gavana Mwangaza anaonekana kuwa peke yake, akikabiliana na mahasimu wake kadhaa wa kisiasa.

Hata hivyo, kila upande unafanya kila uwezalo kuhakikisha umeibuka mshindi kwenye shughuli hiyo, kabla ya mjadala wa kumng’oa mamlakani kiongozi huyo.

Juhudi za kumwondoa mamlakani Bi Mwangaza zimeungwa mkono na uongozi wa vyama kadhaa vya kisiasa katika kaunti hiyo.

Baadhi ya vigogo wa kisiasa ambao wameunga mkono juhudi hizo ni Seneta Kathuri Murungi, wabunge wote 11 katika kaunti, wazee wa Baraza la Njuri Ncheke na Waziri wa Kilimo Mithika Linturi.

Mwishoni mwa Septemba, viongozi wa vyama vya United Democratic Movement (UDA), Devolution Empowerment Party (DEP) na National Ordinary Peoples Empowerment Union (NOPEU), walitangaza kwamba wamejitenga na gavana huyo.

“Kama chama cha kisiasa, tumetangaza vita dhidi ya gavana,” akasema Katibu wa DEP katika kaunti hiyo, Bw Alhaji Mwendia.

Hata kabla ya notisi ya hoja ya kumng’oa mamlakani gavana huyo kuwasilishwa bungeni wiki iliyopita, tayari juhudi za kuwashinikiza wadau zaidi kuunga mkono juhudi hizo zilikuwa zishaanza.

Kama njia ya kutia nguvu juhudi hizo, viongozi wa Meru walianza kumshinikiza Naibu Rais Rigathi Gachagua kuacha juhudi za kuwapatanisha Bi Mwangaza na Naibu Gavana Isaac Mutuma.

“Nimezungumza na viongozi wa Meru ambapo tumeamua kwamba changamoto zinazoikumba Meru zinafaa kusuluhishwa na watu wa Meru. Mimi na Rais hatutaingilia mzozo huo,” akasema Bw Gachagua mapema mwezi wa Oktoba.

Baada ya hakikisho hilo kutoka kwa Bw Gachagua, bunge hilo lilianza kuandaa hoja ya kumtimua Bi Mwangaza.

Akionekana kujawa na wasiwasi, gavana huyo aliiandikia barua Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi na Mahusiano baina ya Serikali akiitaka kuingilia kati mzozo uliopo kati ya serikali yake na Bunge la Kaunti na mvutano uliopo kati yake na naibu gavana.

Kinyume na hapo awali ambapo madiwani wote walishirikishwa kwenye uandaaji wa hoja ya kumtimua mamlakani kiongozi huyo, wakati huu uandaaji huo uliendeshwa kwa siri kubwa.

  • Tags

You can share this post!

Spika wa Seneti akataa wazo la chama chake cha PAA kumezwa...

Bolt yamfuta kazi dereva aliyefungua zipu kimakusudi na...

T L