• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Nafasi ya Joho Azimio kupepeta siasa Pwani

Nafasi ya Joho Azimio kupepeta siasa Pwani

WINNIE ATIENO NA VALENTINE OBARA

HATUA ya kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, kutangaza kwamba atamteua Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, kuwa waziri wa ardhi endapo atashinda urais katika uchaguzi wa Agosti, unatarajiwa kuibua mwelekeo mpya wa kampeni za urais katika eneo la Pwani.

Tangazo hilo lilijiri siku chache baada ya kubainika kuwa, Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, ametengewa wadhifa wa spika wa seneti endapo muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto, utaunda serikali ijayo.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, nyadhifa hizo mbili sasa zinatarajiwa kupigwa darubini katika kampeni za urais wakati Bw Odinga na Dkt Ruto watakapozidi kushindania kura takriban milioni 1.9 zilizo Pwani.

Mnamo wikendi, Bw Joho alipuuzilia mbali nafasi ambayo Bw Kingi ametengewa akisema spika hawezi kuwa na mamlaka ya kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja ikizingatiwa na nyadhifa nyingine za serikalini.

Mchanganuzi wa siasa, Bw Collins Ouma, alikubaliana naye huku akieleza uwezekano wa kauli hiyo kuendelezwa mbele na wanasiasa watakaotaka kushawishi wananchi kuhusu nafasi ya Pwani katika serikali moja au nyingine.

“Wadhifa wa spika ni mkubwa, ndio, lakini mamlaka ya waziri na mchango wake huonekana zaidi kwa wananchi,” akasema.

Kulingana na mtetezi wa haki za kijamii, Bi Topista Juma, uteuzi wa Bw Joho katika nafasi hiyo huenda ukainua Wapwani na kutatua changamoto za mashamba ambalo ni donda sugu ukanda huo.

“Natumai Bw Joho atasuluhisha suala la unyakuzi wa ardhi na kuhakikisha wanawake ambao wananyimwa urathi wa mashamba wanapata haki yao,” akasema, kuhusu endapo Bw Odinga atafanikiwa kushinda urais.

Katika serikali zilizotangulia, baadhi ya Wapwani ambao waliwahi kusimamia idara za ardhi ni Bw Gideon Mung’aro ambaye alikuwa waziri msaidizi wa ardhi katika utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, na Bw Muhammad Swazuri, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi.

Kufikia sasa, haijabainika wazi nafasi ambayo Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya amepangiwa kupewa endapo UDA itaunda serikali ijayo.Bw Joho jana alieleza kuridhishwa kwake na tangazo la Bw Odinga.

“Ninataka kumshukuru Bw Odinga kwa kunichagua wadhifa huo, aliniamini nilipoingia kwenye siasa. Nilikuwa mtoto maskini lakini akanipa nafasi,” alisema Bw Joho.

Wakati uo huo, viongozi wa Pwani wamempongeza Bw Odinga kwa kumchagua kiongozi wa NARC Kenya, Bi Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake.

Wabunge na viongozi wa makundi ya wanawake Pwani walisema kuchaguliwa kwa mwanamke kutainua wanawake kote nchini.Mtetezi wa Haki za Kibinadamu Bi Grace Aloo alisema Bw Odinga ameandikisha historia.

“Huu ni ushindi wetu sote na wanawake wote nchini tutasimama na Bi Karua,” alisema Bi Grace Oloo.

Kwa upande wake, Wakili Ilhan Hisham alisema Bi Karua ni kielelezo bora kwa wanawake.

Bi Terry Mwongeli afisa mkuu wa Shirika la Mawakili Wanawake Nchini (FIDA) alisema kuchaguliwa kwa Bi Karua ambaye ni wakili inaonyesha hatua ambazo wanawake wamepiga.

Mgombea wa uwakilishi wa wanawake Mombasa Bi Zamzam Mohammed alisema Bi Karua ameandikisha historia nchini.

  • Tags

You can share this post!

Tunisia waandamana kuhusu bei za vyakula

Gavana Nyoro ateua mgombea mwenza mwenye tajriba ya matibabu

T L