• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Wakenya kusubiri zaidi kabla kumjua rais mpya

Wakenya kusubiri zaidi kabla kumjua rais mpya

NA JUMA NAMLOLA

WAFUASI wa wawaniaji wakuu wa urais mnamo Alhamisi waliendelea kushikilia roho mikononi, huku makundi ya waangalizi wa uchaguzi yakihimiza amani.

Siku ya tatu tangu Wakenya milioni 14 wapige kura, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliendelea kusubiri fomu zilizotumiwa kuwatangaza washindi kwenye vituo vya kupigia kura.

Fomu hizo zinazojulikana kama 34A, ndizo zinazohitajika, ili zikaguliwe sambamba na nakala zilizotumwa kwa kutumia vifaa vya KIEMS punde baada ya kura za urais kuhesabiwa Jumanne usiku.

Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, Alhamisi alianza upya ujumlishaji wa matokeo, huku akianza na eneo bunge la Webuye Mashariki katika Kaunti ya Bungoma.

Kwenye matokeo hayo, jumla ya kura 30,491 zilipigwa na kukubaliwa huku 249 zikikataliwa.

Wagombea wote wanne wa urais walipata kura ifuatavyo: William Ruto (15,412), Raila Odinga (13,720), George Wajackoya (249) na Mwaure Waihiga (110).

“Tutarejea na kuwatangazia matokeo ya maeneo bunge mengine hadi tukamilishe,” alisema Bw Chebukati baada ya kusoma matokeo hayo.

Tukienda mitamboni, hakuwa amesoma matokeo mengine, na hivyo kubakisha matokeo na maeneo bunge 289 na ya Wakenya wanaoishi nje ya nchi pamoja na wafungwa.

Hatua hiyo mpya ya kulinganisha fomu zote ilichukuliwa wakati vyombo vya habari vikiwa vimebakisha chini ya kura milioni mbili kabla ya kukamilisha ujumlishaji wa kura za vituo vyote.

Kufikia saa kumi na moja, vyombo vya habari vilikuwa vimejumuisha zaidi ya kura 12 milioni, ambapo Bw Odinga alikuwa akiongoza kwa kura zaidi ya 50,000 dhidi ya mpinzani wake mkuu Dkt Ruto.

Awali, kulikuwa na wasiwasi miongoni mwa wafuasi wa wawili hao, huku kila ngome ikijaribu kuonyesha mgombeaji wao alielekea kushinda. Katika jumba la mikutano ya kimataifa la KICC, kulikuwa na zulia jekundu huku magari ya serikali yakifika.

Hali ilikuwa sawa na hiyo kwa upande wa Kenya Kwanza, katika Chuo Kikuu cha Catholic, Karen, Nairobi, ingawa hakukutolewa kauli yoyote kuhusu sababu ya kufanya hivyo.

Makundi ya waangalizi wa uchaguzi, asubuhi yalitoa taarifa ambapo kwa kiasi kikubwa yalihimiza Wakenya wawe wavumilivu kiasi.

Kiongozi wa kundi la waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw Jakaya Kikwete, alishauri kuwe na utulivu na uvumilivu.

“Kundi letu lina wasiwasi kuhusu kuendelea kuchelewa kwa matokeo. Tunawaambia wanasiasa wote na wadau wengine, hasa Wakenya wenyewe, waendelee kudumisha amani. Wale watakaohisi kuwa hawajatendewa haki, tunawashauri watumie njia zinazotambuliwa na sheria, ambazo ni pamoja na kwenda mahakamani,” akasema Bw Kikwete.

Rais huyo wa zamani wa Tanzania alieleza masikitiko ya jopo lake kwamba, katika vituo vya kupigia kura, waangalizi na maajenti wa vyama au wagombeaji walikuwa mbali sana na walipokuwa maafisa wa kusimamia uchaguzi.

“Kwa fikira zetu, tulitarajia kuwa maajenti wangekuwa karibu wakati wa kuwatambua wapigakura, ili wawe na kauli na washiriki kikamilifu wakati wa utambuzi. Badala yake, tuliona watu wakiingia na kujitambulisha kwa maafisa wa uchaguzi. Maajenti walitazama tu wakati wa utumbukizaji kura ndani ya masanduku,” akasema.

Waangalizi hao pia walipata malalamishi kutoka kwa vijana, ambao wengi walihusishwa tu kama makarani wa kura kati ya shughuli nyingine, badala ya kuwa miongoni mwa wanasiasa wa kupigiwa kura.

Jopo la Umoja wa Afrika (AU) pamoja na COMESA, liliihimiza IEBC na taasisi nyingine zinazohusika na shughuli ya uchaguzi, ziimarishe uwazi na kuwafahamisha Wakenya kila mara kuhusu hatua zinazochukuliwa kabla ya kumjua rais wao wa tano.

  • Tags

You can share this post!

Serena abanduliwa Canadian Open

Ruweida aweka historia akichukua kiti cha ubunge

T L