• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Niko tayari kuwa mgombea mwenza wa Raila- Munya

Niko tayari kuwa mgombea mwenza wa Raila- Munya

Na ALEX NJERU

WAZIRI wa Kilimo, Bw Peter Munya, amesema hatakataa kuwa mgombea mwenza wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao. Bw Munya

alisifia mdahalo unaoendelea kuhusu uwezekano wake kuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga, kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Akihutubu jana alipofungua Mradi Mpya wa Unyunyizaji Maji wa Makanyanga katika Kaunti ya Tharaka-Nithi, Bw Munya alisema kuwa ingawa nia yake ni kuwania ugavana katika Kaunti ya Meru, bado kuna uwezekano akachukua nafasi ya ugombea-wenza ikiwa itajitokeza.

Mradi huo ulijengwa kwa gharama ya Sh260 milioni. “Ninafurahia mdahalo huo kwani unaashiria dalili za nia njema kutoka kwa viongozi wa ukanda huu,” akasema Bw Munya. Alisema eneo la Mlima Kenya litahakikisha litakuwa katika serikali ijayo na litafuata mwelekeo litakaopewa na Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Munya alikuwa akijibu rai za viongozi wa Tharaka Nithi kumtaka kuwania nafasi ya kitaifa. Viongozi hao waliongozwa na Dkt Mutegi Kabisani, anayelenga kuwania ubunge katika eneo la Tharaka, Bi Mercy Kirito (Chuka/Igambang’ombe) na Dkt Kunga Ngeeche, anayelenga kuwania useneta.

Watatu hao wamesema watawania nyadhifa hizo kwa kutumia tiketi ya chama cha PNU, kinachohusishwa na Bw Munya. Dkt Kabisani aliwarai wenyeji wa Mlima Kenya kumuunga mkono Bw Munya kuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga.

“Nawarai wanasiasa wa Mlima Kenya kumuunga mkono Bw Munya kwa nafasi ya mgombea-mwenza ili eneo hili liwe kwenye serikali ijayo. Nina uhakika kwamba Bw Odinga ndiye ataibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha urais,” akasema Dkt Kabisani.

You can share this post!

FAO yaonya kuhusu uvamizi wa nzige

Haaland afunga mabao mawili na kusaidia Dortmund kupepeta...

T L