• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
FAO yaonya kuhusu uvamizi wa nzige

FAO yaonya kuhusu uvamizi wa nzige

Na GEOFFREY ONDIEKI

SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), limeonya kuhusu uvamizi mpya wa nzige nchini Kenya na Ethiopia kuanzia kati kati ya mwezi huu wa Desemba.

Shirika hilo linaonya kuwa wadudu hao hatari wanataga mayai, ambayo yataanguliwa na kuunda jeshi la nzige kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia katika wiki zijazo.Haya yanajiri miezi michache baada ya serikali ya Kenya kutangaza kuwa nchi imekabili uvamizi wa nzige.

Kwa mujibu wa FAO, makundi madogo madogo yaliyokomaa ambayo yalivamia Kaskazini Mashariki mwa Kenya kutoka Somalia katika wiki ya kwanza ya Novemba, yamerejea Kusini mwa Ethiopia, ambako shughuli za udhibiti zinaendelea.

“Makundi madogo madogo yaliyokomaa kutoka Kaskazini Mashariki mwa Somalia yalitua katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Makundi hayo ni hatari na yanahitaji hatua za haraka ili kuyadhibiti,” ikasoma ripoti.

Kadhalika, ripoti hiyo pia ilisema kuwa nchi hiyo jirani tayari imeanza kushuhudia athari za wadudu hao huku kila majani ya miti yakitafunwa na nzige hao.“Baadhi ya athari za wadudu hao zitadumu kwani nzige wadogo wadogo wataibuka na kukomaa.

Wakati mimea inakauka, kundi hilo litahamia Kusini mwa Ethiopia na Kusini mwa Somalia ambapo wanaweza kuanza kuonekana Kaskazini Mashariki mwa Kenya na kuenea Magharibi mwa kaunti za Kaskazini.”

Kaunti zilioathiriwa

Kaunti ya Samburu, ambayo ilikuwa mojawapo ya kaunti zilizoathiriwa na wadudu hao waharibifu katika mkumbo wa kwanza na wa pili wa uvamizi, sasa imejiandaa kwa uvamizi huu wa mkumbo wa tatu, asema Afisa Mkuu wa Mipango Maalum katika Kaunti, Bw Daniel Lesaigor.

Bw Lesaigor alibainisha kuwa kaunti hiyo imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo wataalamu watakaofanya utafiti wakishirikiana na Wizara ya Kilimo ili kupambana na wadudu hao hatari.“Bila kuingilia kati, wadudu hao wataleta maadhara nchini na kupunguza uzalishaji wa chakula.

Japo hatujui idadi ya nzige hao, tunashirikiana na wataalamu husika ili kuwa tayari kupambana nao,” akasema Bw Lesaigor.Aliongeza kuwa wenyeji wana teknolojia itakayowasaidia kuwatafuta wadudu hao iwapo uvamizi mpya utaripotiwa.

Mnamo Juni mwaka huu, serikali ilitenga Sh1.8 bilioni kusaidia katika kupambana na nzige ambao walivamia maeneo ya Kaskazini mwa nchi ambalo pia lilikuwa likikumbwa na janga la njaa.Tangu 2019, wadudu hao waharibifu wamesababisha uharibifu mkubwa katika sekta ya kilimo na hata kupunguza uzalishaji wa chakula katika nchi zaidi ya 20 Afrika Mashariki, Afrika Magharibi, Asia Magharibi na Asia Kusini.

Wadudu hao hula majani, maua, matunda, mbegu na chochote chenye kijani.Kulingana na FAO, kundi moja tu linaweza kuwa na nzige milioni 40 na kula chakula kinachoweza liwa na zaidi ya watu 35,000 kwa siku.

You can share this post!

Spika apuuza hatua ya EACC kuzima uteuzi wa naibu gavana...

Niko tayari kuwa mgombea mwenza wa Raila- Munya

T L