• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Nilimnoa kisiasa Ruto na haniwezi, Raila sasa ajigamba

Nilimnoa kisiasa Ruto na haniwezi, Raila sasa ajigamba

NA BY IAN BYRON

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amemtaja Naibu Rais William Ruto kuwa “mwanasiasa mdogo” ambaye hana ajenda yoyote muhimu kwa Wakenya.

Jana, Bw Odinga alimwambia Dkt Ruto kujiandaa kwa kivumbi kikali kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kwenye hotuba fupi kwa wafuasi wake katika Shule ya Msingi ya Kanga, Kaunti ya Migori, Bw Odinga alimpuuzilia mbali Dkt Ruto kwa mtindo wake wa “kujipiga kifua”, akimtaja mwanasiasa wa kiwango cha chini mwenye uchu na tamaa ya mamlaka.

Vile vile, alimlaumu Dkt Ruto kwa kumtaja kuwa ‘Mradi wa Serikali’ kutokana na handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 2018.

Tayari, Rais Kenyatta ametangaza atamuunga mkono Bw Odinga kuwa mrithi wake.

“Yeye (Ruto) amekuwa na mazoea ya kunitaja kuwa mradi wa kisiasa.

Ikiwa yeye ni mwanamume kamili, basi awe tayari kukabiliana nami kwenye uchaguzi wa Agosti. Atajua kwamba alikuwa mwanafunzi wangu wa kisiasa kwa wakati mmoja,” akasema Bw Odinga huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Seneta Ochillo Ayacko (Migori), mbunge Junet Mohamed (Suna Mashariki) kati ya viongozi wengine.

Kigogo huyo aliwarai wenyeji wa Migori kujihami kwa kura zao ili kumwezesha “kukabiliana na adui anayetishia kuirejesha nchi nyuma.” “Niliwaambia muwe tayari kwa safari yetu ya kuingia Ikulu. Tuko tayari kukabiliana na wapinzani wetu (Kenya Kwanza) ambao lengo lao ni kuvuruga uchumi wetu,” akasema.

Akaongeza: “Kuna vyama kadhaa ambavyo viko tayari kushirikiana nasi ili kutuwezesha kuchukua uongozi.” Kauli yake iliungwa mkono na Bw Mohamed, aliyesema kuwa Wakenya wanapaswa kujiyatarisha kwa muungano mkubwa wa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Kalonzo alisaliti Mudavadi,...

UDA kuiga IEBC kuandaa uteuzi

T L