• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Raila afufua mapambano

Raila afufua mapambano

NA CECIL ODONGO

KINARA wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ametangaza mapambano makali dhidi ya utawala wa Rais William Ruto imeanza kuwakandamiza maafisa waliokuwa waaminifu kwa utawala uliopita.

Hapo jana Alhamisi, Bw Odinga alidai kuwa utawala wa Rais William Ruto una njama ya kumhujumu na kumwadhibu aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi Nchini George Kinoti. Pia alisema serikali imeanza kubadili nia kuhusu ahadi ilizotoa wakati wa kampeni hasa za kupunguza gharama ya maisha.

Waziri huyo mkuu wa zamani alikashifu Rais, akisema amejawa na kisasi kwa kuwa kuna mpango unaondelea wa kuwawinda maafisa katgka utawala uliopita ambao Rais Ruto aliwaona kama maadui kwenye azma yake ya kuingia ikulu.

Kinara huyo wa ODM alisema Rais Ruto anamlenga Bw Kinoti katika uchunguzi ambao unaendelea kuhusu watu ambao wanaodaiwa kutoweka na kuuawa kinyama akiwemo raia wawili kutoka India. Bw Odinga alisema wawili hao waliletwa nchini wakati ambapo kampeni ilikuwa ikiendelea na kambi ya Rais Ruto.

“Tunasikitishwa na mkondo ambao uchunguzi kuhusu mauaji ya kinyama yaliyotokea umechukua. Ni dhahiri kuwa uchunguzi huu unalenga aliyekuwa mkuu wa DCI George Kinoti na maafisa wachache wa polisi,” akasema Bw Odinga.

Alikuwa akizungumza katika afisi zake za Capitol katika kikao na wanahabari ambapo aliwakabidhi tikiti baadhi ya wanasiasa ambao watawania kura katika chaguzi ndogo za Bungoma na wadi ya Utawala, Kaunti ya Nairobi.

“Kisasi cha William Ruto dhidi George Kinoti na DCI kilianza hata kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu kufanyika. Ruto anaamini kuwa utawala wa UDA umempa fursa nzuri ya kuwaadhibu maafisa wa usalama ambao amekuwa na kisasi nao. Sisi hapa tunasema hatutakubali mambo yachukue mwelekeo huo,” akaongeza Bw Odinga.

Wakati alipokuwa akitangaza Baraza lake la Mawaziri mnamo Septemba 27, Rais Ruto alitangaza kuwa Bw Kinoti alikuwa amemwandikia barua ya kujiuzulu kutoka kwa wadhifa wake.

Hatua hiyo ilipisha mchakato wa kuteua DCI mwengine ambao ulikamilika mnamo Oktoba 15 baada ya kumteua mshikilizi wa wadhifa huo kwa sasa Amin Mohamed. Bw Mohamed alikuwa kati ya watu 10 ambao majina yao yalipendekezwa na Tume ya Huduma za Polisi (NPS) baada ya kufanyiwa mahojiano.

Waziri huyo mkuu wa zamani alikariri kuwa kupotea kwa njia tatanishi kwa raia kutoka India ambao walikuwa sehemu ya kampeni za Rais Ruto hakufai kutumika kulipa kisasi dhidi ya Bw Kinoti na maafisa wengine wa polisi.

“Raia hao walikuwa wanastahili kuwa hai kwa sababu ni binadamu. Tuna matumaini kuwa haki itatendwa kwenye kesi yao. Hata hivyo, uchunguzi unapoendelea, serikali inastahili kuweka nguvu hizo katika mauaji mengine tatanishi ambayo yametokea hapo awali,” akasema Bw Odinga.

Mnamo Oktoba 23, mifupa, nguo na kamba zilizoaminika kuwa za Wahindi hao wawili zilipatikana msituni Aberdare to kusafirishwa kufanyiwa uchunguzi ambao baadaye ulibaini kuwa vifaa hivyo havikuwa vyao.

Maafisa 12 ambao walitoka kikosi cha Kitengo Spesheli cha Kukabiliana na Uhalifu (SSU), wamehojiwa wakati wa uchunguzi kuhusu utekaji nyara wa wawili hao. Rais Ruto aliamrisha kikosi hicho kivunjwe kutokana na kuhusishwa kwake na utekaji nyara na mauaji ya kiholela.

Kati ya vifo vingine ambavyo Bw Odinga alitaka utawala wa Rais Ruto ufanyie uchunguzi ni mauaji ya baadhi ya watu waliostahili kutoa ushahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Nchini (ICC) na wale ambao walikosana na Rais alipokuwa akihudumu kama Naibu Rais.

Kati ya wale ambao alitaka uchunguzi kuhusu mauti yao uchunguzwe ni Meshack Yebei, wanahabari John Kituyi, Walter Barasa, Philip Koech na afisa wa cheo cha sajini Kipyegon Kenei. Wengine ni George Thuo, Naftali Irungu , Njuguna Gitau, George Njoroge, wakili Paul Ndung’u na aliyekuwa menega wa Teknojia kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) Chris Musando.

Bw Odinga pia jana Alhamisi alipinga pendekezo la Rais la kuongeza ushuru ambao Wakenya wanatozwa kufadhili miradi ya Jubilee, akisisitiza raia wanastahili kushauriwa na ushuru huo unastahili kuoana na uwakilishi.

Rais Ruto wiki jana aliitaka Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) ipanue mawanda yake na ihakikishe kuwa kila Mkenya ambaye amefikisha umri wa miaka 18 analipa ushuru.

  • Tags

You can share this post!

Kamati yapinga pendekezo Hospitali ya Mama Lucy ifungwe

Usiumize wafuasi wangu – Raila

T L