• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
Raila aingia boksi ya Ruto

Raila aingia boksi ya Ruto

BENSON MATHEKA, CHARLES WASONGA Na KASSIM ADINASI

HATUA ya kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ya kuruhusu washirika wake kumkumbatia Rais William Ruto inaonyesha ameacha misimamo mikali dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza alivyotaka kiongozi wa nchi.

Viongozi na wakazi wa ngome ya Bw Odinga ya Nyanza, walimkaribisha kwa wingi Rais Ruto katika ziara aliyofanya kaunti za Homa Bay na Siaya mnamo Ijumaa na Jumamosi.

Hii ni baada ya Bw Odinga anayezuru Afrika Kusini, mnamo Alhamisi kukutana na viongozi kutoka ngome yake na kuwaagiza wamkaribishe rais, tofauti na waliposusia hafla yake kaunti ya Homa Bay mwaka jana.

Gavana wa Siaya, Jame Orengo, jana aliwasilisha “salamu” za Bw Odinga kwa Rais Ruto katika hafla ya kumkaribisha nyumbani Waziri wa Habari Eliud Owalo huko Rarieda.

“Nimezungumza na Raila muda wa saa moja iliyopita na akaniambia nikwambie amekukaribisha na ujihisi kuwa nyumbani,” alisema Bw Orengo.

Rais Ruto amekuwa akisisitiza kuwa kipindi cha kampeni za uchaguzi kimeisha na ni wakati wa kufanya kazi na viongozi wote waliochaguliwa.

Mapema mwaka huu 2023, Bw Odinga alitangaza kuwa amewaagiza magavana wa Azimio kushirikiana na serikali ili kunufaika na maendeleo katika kaunti zao, lakini akawaonya wasimezwe na serikali.

Anapozuru katika kaunti za upinzani, Rais Ruto amekuwa akitangaza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo wadadisi wanasema inaweza kufanya magavana kumkaidi Bw Odinga.

Mbinu hii ya Rais Ruto imemfanya Bw Odinga kuwapa nafasi washirika wake kushirikiana na serikali.

Aidha, Bw Odinga anaonekana kukubali mpango wa Rais Ruto ya kubuniwa kwa kiongozi rasmi wa upinzani Bungeni japo kiongozi wa nchi amesisitiza halengi mtu binafsi katika pendekezo lake.

Rais pia amependekeza mabadiliko katika Katiba ambayo Bw Odinga anaonekana kuchangamkia na majuzi akiwa Mombasa alimwambia Rais Ruto “amtafute wajadili” mabadiliko hayo.

Raila pia anaonekana kuacha mikutano aliyoacha kufanya katika ngome zake kuwapa wafuasi wake mwelekeo baada ya kushindwa kudai hakukubali uamuzi wa Mahakama ya Upeo ulioidhinisha ushindi wa Rais Ruto hatua ambayo inaashirika kukubali serikali ya Kenya Kwanza.

Miradi ya maendeleo ambayo Rais William Ruto amekuwa akiahidi kutekeleza katika ngome za kiongozi wa upinzani Raila Odinga inaonekana kama mbinu zake za kumwingiza boksi waziri mkuu huyo wa zamani.

Tangu alipoingia mamlakani Septemba 13, mwaka jana Dkt Ruto amekuwa akifanya ziara katika maeneo ya Ukambani, Pwani, Magharibi na Nyanza akiahidi serikali yake itatekeleza miradi kadha ya kuchochea maeneo katika maeneo hayo.

Hii ni licha ya kwamba wakazi wa maeneo hayo walimpa kura nyingi Bw Odinga, ambaye alikuwa mpinzani wake mkuu, katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wadadisi wanasema ziara za Dkt Ruto na “minofu ya maendeleo” anayotoa kwa wakazi ni sehemu ya mikakati yake ya kuvuwatia viongozi na wakazi wa ngome za Raila upande wake.

Tangu mwishoni mwa mwaka jana, Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza haifai kubagua Ukambani, Pwani, Magharibi na Nyanza, kimaendeleo kwa misingi ya kuwa ngome cha Azimio la Umoja-One Kenya.

“Ni wajibu wa serikali iliyoko mamlakani kusambaza maendeleo katika sehemu zote za nchini, zikiwemo ngome zetu kama Azimio. Wafuasi wetu hawafai kuadhibiwa kwa kunyimwa maendeleo eti kwa sababu walinipigia kura ilhali wao pia ni walipa ushuru. Tutaendelea kupigania maendeleo kwa watu wetu katika msururu wa mikutano tutakayofanya katika ngome zetu za Magharibi, Pwani, Ukambani na Nyanza siku zijazo,” akasema alipohutubia wafuasi wa Azimio katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi, Desemba 7,2022.

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Ndoa ni nipe nikupe, hakuna kuwa kupe...

Brighton waduwaza Liverpool kwa kuipokeza kichapo cha 3-0...

T L