• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
‘Raila alipanga kutenga Pwani na Kenya’

‘Raila alipanga kutenga Pwani na Kenya’

Na MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Wikileaks limefichua kwa undani makubaliano yaliyofanywa kati ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga na viongozi wa Kiislamu kabla Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Ijapokuwa ilifahamika Bw Odinga alikuwa na maelewano na Shirikisho la Viongozi wa Kiislamu Kitaifa (NAMLEF) kabla ya uchaguzi huo, wengi hawakufahamu yalihusu nini.

Katika nakala zilizotolewa na Wikileaks mnamo Jumapili, ilifichuka kuwa Bw Odinga alikuwa ameahidi kuwa endapo angeshinda katika uchaguzi huo, angewezesha eneo zima la Pwani kuwa huru na kujitawala, isipokuwa kijeshi pekee.

Wakazi wa Pwani kwa miaka mingi wamekuwa wakishinikiza ukanda huo mzima uwe huru kutoka Kenya, wakilalamika kudhulumiwa na kutengwa kimaendeleo na serikali kuu.

Hii ni licha ya kuwa eneo hilo lina rasilimali tele za mali-asili na za kiuchumi kama vile bandari na maeneo makuu ya utalii.

Mbali na hayo, imefichuka pia Bw Odinga aliahidi viongozi wa Kiislamu kwamba maeneo ambayo yana idadi kubwa ya waumini wa dini hiyo yangeruhusiwa kutumia sheria za Kiislamu kiutawala.

Hii ingemaanisha kuwa, shughuli mbalimbali ambazo ni haramu kwa Waislamu zingepigwa marufuku katika sehemu hizo za nchi, kwa mfano uuzaji au unywaji wa pombe na nyama ya nguruwe.

Mbali na Pwani, sehemu nyingine za nchi ambapo kuna idadi kubwa ya Waislamu ni Kaskazini Mashariki.

Kwa mujibu wa Wikileaks, makubaliano hayo yalitiwa sahihi na Bw Odinga, Mwenyekiti wa NAMLEF wakati huo Abdullahi Abdi, na Waziri wa Utalii Najib Balala.

Katika uchaguzi huo wa 2007, Rais Mstaafu Mwai Kibaki ndiye aliyetangazwa mshindi katika hali tatanishi ambayo ilisababisha vita vilivyopelekea zaidi ya watu 1,000 kuuawa kikatili na maelfu wengine wakafurushwa makwao.

You can share this post!

Corona haitambui mamlaka, waliokuwa Ikulu kupimwa

Mchina ndani kwa kuuza vifaa feki vya corona

adminleo