• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Raila kupokea wabunge wa ANC Murang’a

Raila kupokea wabunge wa ANC Murang’a

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa Azimio la Umoja Raila Odinga leo Jumamosi anatarajiwa kutumia mkutano wake uwanjani Ihura, Kaunti ya Murang’a, kupokea rasmi wabunge kutoka chama cha Amani National Congress (ANC) chake Musalia Mudavadi.

Miongoni mwa wabunge wa ANC wanaotarajiwa kutangaza rasmi kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja ni Bw Tindi Mwale (Butere) na Bw Titus Khamala (Lurambi), kulingana na wandani wa Bw Odinga waliozungumza na Taifa Leo.

Wawili hao, Alhamisi asubuhi walikutana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli na baadaye jioni kufanya kikao cha faragha na Bw Odinga.

Tayari wabunge watano wa ANC; Ayub Savula (Lugari), Christopher Aseka (Khwisero), Oku Kaunya (Teso Kaskazini), Peter Nabulindo (Matungu) na Godfrey Ototsi (Maalumu) walishahamia ODM na chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kinachohusishwa na waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.

Baada ya Bw Mudavadi na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kutangaza kuungana na Naibu wa Rais William Ruto, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wanaonekana kutaka kuwadhoofisha viongozi hao kwa kuwapokonya wandani wao.

Mwakilishi wa Wanawake wa Trans Nzoia Janet Nangabo ambaye awali alikuwa mwandani wa Dkt Ruto pia amehamia DAP-K.

Alhamisi, madiwani 20 kutoka kaunti za Magharibi waligura ANC na Ford Kenya na kujiunga na chama cha DAP-K kinachoongozwa na mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi.

Chama cha ANC kilikuwa na jumla ya maseneta na wabunge 17 lakini sasa kimesalia na chini ya watano.

Bw Mudavadi amesalia na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na wabunge Malulu Injendi (Malava), Vincent Gemose (Hamisi) na Beatrice Adagala (Mwakilishi wa Wanawake wa Vihiga).

Chama cha Ford Kenya kimesalia na mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa, Ferdinand Wanyonyi (Kwanza) na Majimbo Kalasinga (Kabuchai).

Bw Kalasinga aligura Ford Kenya na kujiunga na United Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto miezi mitatu baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Machi 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo James Lusweti aliyefariki Desemba 2020.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Bw Atwoli ndio wamekuwa wakitumiwa na Bw Odinga kushawishi viongozi waliochaguliwa kwa tiekti ya ANC na Ford Kenya 2017 kujiunga na Azimio la Umoja.

Nao mabwanyenye kutoka eneo la Mlima Kenya wamekuwa wakikutana na viongozi wa jamii mbalimbali nchini kujaribu kuwashawishi kujiunga na Azimio la Umoja.

Jana Ijumaa, wandani wa Naibu wa Rais Ruto walitumia mkutano wao katika Kaunti ya Bungoma kushambulia chama cha DAP-Kenya.

Walidai kuwa chama cha DAP-K kiliundwa kumaliza ushawishi wa Bw Wetang’ula katika eneo la Magharibi baada ya kukataa kuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Naibu wa Rais William Ruto analenga kunyakua mamilioni ya kura kutoka eneo la Magharibi kupitia kwa Mabw Mudavadi na Wetang’ula.

Bw Odinga pia analenga kutumia ziara yake ya leo katika kaunti ya Murang’a kujipigia debe.

You can share this post!

Vuguvugu la Umoja Mlimani lasambaratika

DOUGLAS MUTUA: Umaarufu wa Kiswahili na jinsi...

T L