• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Ushuru wa ziada utumike kuokoa raia wa tabaka la chini

TAHARIRI: Ushuru wa ziada utumike kuokoa raia wa tabaka la chini

NA MHARIRI

WIKI jana, serikali ilitangaza mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ambapo ilisema ilizidi malengo yake kwa takribani Sh200 bilioni.

Mafanikio hayo japo ni mazuri kwa sababu yatasaidia serikali kutimiza mipango yake ya kifedha, kwa upande mwingine yana maana kuwa raia wanafinywa kwa kutozwa ushuru wa juu.

Hakika ni kutokana na ushuru wa juu ambapo bidhaa nyingi za kimsingi zimeongezeka bei kiasi cha kutisha raia wa kawaida.

Naam si kweli kuwa tatizo la gharama ya maisha limetokana na ushuru wa juu pekee. Sababu nyingine ni kama vile janga la corona, kiangazi cha muda mrefu kilichoharibu mchakato wa kuzalisha chakula, na mgogoro unaoendelea nchini Ukraine.

Katika tahariri hii, tunachungua hasa ushuru kama sababu kuu ya kupanda kwa gharama ya maisha. Kwa mfano, tangu serikali ya Jubilee ichukue ususkani, takribani bidhaa zote zikiwemo za kimsingi kama vile unga, zinatozwa ushuru, tena wa juu.

Katika utawala uliotangulia huu uliopo, baadhi ya bidhaa za kimsingi kama vile unga wa mahindi, zilipunguziwa ushuru au hata tozo hilo kuondolewa kabisa. Hilo lilifanya maisha yawe rahisi. Utawala wa leo unatoza ushuru hata mgao wa wawekezaji katika vyama vya ushirika yaani Saccos! Hata akaunti za benki zinatozwa ada ya kila mwezi.

Waama, zipo serikali zilizofuata sera kama hii ya Jubilee ambazo baadaye raia wake walinufaika pakubwa maadamu kodi hizo za juu zilitumika vizuri bila ufisadi. Ni udikteta wenye makusudio ya kumfaa raia wa kawaida.

Lakini katika muktadha wa Kenya, sehemu kubwa ya ushuru huu wa Sh2 trilioni uliokusanywa na mamlaka ya ushuru ya KRA, itatumika kulipa madeni huku sehemu nyingine ikipotelea mifukoni mwa watu binafsi.

Pesa kama hizo ndizo zinazofaa kuwaokoa raia wanaoteswa na janga la njaa linalokumba sehemu kubwa ya taifa hili na nchi nyingine barani Afrika na hata duniani.

Serikali ingetenga kiasi cha Sh10 bilioni, kwa mfano, kutoa ruzuku kwa unga wa mahindi ambao kwa sasa pakiti moja ya kilo mbili inauzwa kwa Sh200.

Tahariri hii haina dhamira ya kuzuia serikali kupanua njia zake za kutoza ushuru, bali ni muhimu bidhaa za kimsingi ziondolewe ushuru.

Wanaokwepa kulipa ushuru wakabiliwe na pesa za ziada zinazopatikana kutokana na kodi hiyo ya juu zitumike kuboresha huduma za umma kama vile afya, elimu na kukabili majanga.

You can share this post!

Raila kuzuru Pwani telezi

Gari la kampeni za Orengo lateketea jenereta ilipolipuka

T L