• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Ruto aahidi wakazi wa Lamu vinono punde akiwa rais

Ruto aahidi wakazi wa Lamu vinono punde akiwa rais

NA KALUME KAZUNGU

NAIBU wa Rais, Dkt William Ruto amesema jukumu lake la kwanza atakapochaguliwa rais hapo Agosti mwaka huu ni kuhakikisha wavuvi walioathiriwa na Mradi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) wanalipwa fidia yao ya Sh1.76 bilioni.

Jumla ya wavuvi 4,734 wa Lamu kwa zaidi ya miaka mitano sasa wamekuwa wakisubiri fidia yao licha ya Mahakama Kuu mjini Malindi kuamuru serikali kuwalipa wavuvi hao Sh1.76 bilioni mnamo Mei, 2018 baada ya kubainika kuwa sehemu za uvuvi za Lamu ziliathiriwa pakubwa na ujenzi wa Lapsset.

Kufikia sasa fedha hizo hazijatolewa.

Akizungumza alipoongoza kampeni za kupigia debe muungano wa Kenya Kwanza Ijumaa, Bw Ruto ambaye pia ni kiongozi wa chama cha UDA, alieleza kutamaushwa kwake na jinsi serikali ya sasa inavyowakandamiza wavuvi na hata kuwanyima haki yao ya fidia.

Bw Ruto aliwasihi wakazi wa Lamu kumpigia kura na kumwezesha kuingia ofisini Agosti 9, akishikilia kuwa atakalofanya kwanza akiingia mamlakani ni kuona kwamba fedha za fidia kwa wavuvi wa Lamu zinatolewa mara moja.

“Ninafahamu kwamba serikali ya sasa bado haijawalipa wavuvi wa Lamu fedha zao baada ya kuathiriwa na Lapsset. Azma yangu ya kwanza ni kuhakikisha mumelipwa fedha zenu nitakapoingia mamlakani Agosti 9. Hizo ni fedha zenu n ani vyema ikiwa mtalipwa,” akasema Bw Ruto.

Alisema mbali na fidia ya Lapsset, serikali ya Kenya Kwanza pia inanuiwa kutenga kima cha Sh50 bilioni kuinua wanabiashara wa biashara ndogondogo.

Sh100 bilioni nyingine pia zitatengwa ili kuinua wakulima kupitia mbolea, mbegu za kisasa miongoni mwa masuala mengine yatakayohakikisha usalama wa chakula unaimarishwa nchini.

Akigusia suala la ajira, Bw Ruto a;liikashifu serikali kwa ubaguzi katika kuajiri vijana wa Lamu hasa katika masuala ya kitengo cha polisi, jeshi na walimu.

Alisema lengo lake atakapoingia madarakani ni kuhakikisha vijana zaidi ya 5000 wa Lamu wanaajiriwa.

“Watu wamekuwa wakija hapa kuajiri vijana watatu kama polisi, kumi kama wanajeshi na kumi na tano kama walimu. Hilo si jambo jema. Sisi tukiunda serikali tutahakikisha zaidi ya vijana 5000 wa hapa wanaajiriwa ili kujisikia pia ni miongoni mwa wakenya wengine,” akasema Bw Ruto.

Pia aliahidi kuhakikisha kila mwananchi, hata yule wa tabaka la chini anafadhiliwa katika mpango wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) kabla ya Disemba mwaka huu.

Kwa upande wake, kinara Mwenza, Moses Wetangula ambaye pia ni kiongozi wa Ford-Kenya, aliwarai wakazi wa Lamu kumchagua Naibu wa Rais, William Ruto kuongoza nchi hii ifikapo Agosti 9 mwaka huu.

Alisema ni kupitia serikali ya Kenya Kwanza ambapo Lamu itanasuliwa kutoka kwa ubaguzi wa muda mrefu.

“Lamu ni kaunti muhimu inayochangia pakubwa maendeleo ya hapa nchini. Hapa Lamu tunajivunia utalii, uvuvi, bandari ya Lapsset, gesi na mafuta. Lazima watu wa Lamu wahusishwe kimalilifu na kuona kwamba wanafaidi rasilimali zitokazo hapa. Haya yote yatatimia iwapo tutamchangua Bw Ruto kuongoza nchi hii ifikapo Agosti 9 mwaka huu,” akasema Bw Wetangula.

Wengine walioandamana na Bw Ruto kwenye ziara ya Lamu ni kinara mwenza wa Kenya Kwanza na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, gavana wa zamani wa eneo hilo, Issa Timamy, Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale, Seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki, Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa, Gavana wa zamani wa Tana River, Hussein Dado, seneta wa zamani wa Mombasa, Hassan Omar, Seneta wa Lamu, Anwar Loitiptip, Mbunge wa Lamu Mashariki, Athman Sharif na wengineo.

  • Tags

You can share this post!

Afueni serikali ikipunguza pakubwa bei za mbolea

Wapigakura wafu 250,000 kutupwa

T L