• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Ruto aapa kuandama Rais Kenyatta

Ruto aapa kuandama Rais Kenyatta

NA WALTER MENYA

NAIBU Rais William Ruto ameapa kuunda tume ya mahakama kuchunguza vitendo na sera za Rais Uhuru Kenyatta iwapo atashinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, hatua ambayo imemfanya ashambuliwe na viongozi wa Jubilee.

Dkt Ruto pia anajiandaa kufuta sera kadhaa za Rais Kenyatta akishinda urais na hata kuashiria kwamba hatachelea kumwandama rais atakapoondoka mamlakani.

Katika manifesto ya Muungano wa Kenya Kwanza aliyozindua Alhamisi usiku, Dkt Ruto anasema iwapo Kenya Kwanza itashinda uchaguzi mkuu wa Agosti, itaunda jopo la kuchunguza kutoweka kwa watu na ukiukaji wa haki za binadamu.

Aidha, manifesto inasema kwamba serikali ya Kenya Kwanza itachunguza kutekwa nyara kwa serikali na watu wenye ushawishi hatua ambayo inaweza kumaanisha kwamba watamwandama rais na jinsi alivyoongoza serikali.

Vile vile, aliapa kuunda majopo manane na tume kuchunguza na kubadilisha sera za Rais Kenyatta.Chini ya mada ya “Kumaliza Utekaji nyara wa Serikali,” Dkt Ruto anaahidi kuanzisha “ ndani ya siku 30, uchunguzi wa mahakama wa umma kubaini kiwango cha utekaji wa serikali na watu wenye ushawishi na kutoa mapendekezo.”

Ingawa amekuwa naibu rais tangu 2013, naibu rais alijitenga na serikali baada ya kutofautiana na Rais Kenyata.

Hii imemfanya Dkt Ruto kulaumu serikali ya Jubileee kwa kuthibitiwa na anaodai ni mitandao, walaghai na watu wanaoharibu uchumi ambao amekuwa akilaumu kwa kupanda kwa gharama ya maisha.

“Tunajua kwamba kwa miongo minne, mfumo wetu wa uchumi una dosari. Swali ni kwani tumekuwa katika njia hii, kwa nini serikali haikufuata kauli mbiu yetu ya kubadilisha uchumi, kwa nini tulichagua kutengeneza bunduki lakini sio nguo. Jibu ni kuunganisha nguvu za kisiasa na uchumi,” inasema manifesto ya Kenya Kwanza.

Mnamo Ijumaa, washirika wa Naibu Rais walifafanua kuhusu mapendekezo hayo na kumlaumu Rais kwa kutumia sera za serikali kwa manufaa yake jambo ambalo wanasema tume itachunguza wakishinda uchaguzi na kuingia mamlakani.

“Kutekwa kwa serikali kulemaza uchumi wetu. Tatizo ni kwamba Rais na washirika wake kwa miaka kumi iliyopita wameunda sera na kufanya maamuzi ya kunufaisha biashara zake. Sawa na Guptas wa Afrika Kusini, kila kitu kimepangwa kunufaisha biashara za kibinafsi za wale walio mamlakani,” akasema mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Kulingana na Bw Nyoro, sekta muhimu za uchumi kwa wakati huu zinathibitiwa na familia chache zenye ushawishi na hii ndio sababu serikali ya Kenya Kwanza inatoa mapendekezo ya kufanya uchunguzi.

“Aina ya ulafi ambao tumeshuhudia katika miaka saba iliyopita ni wa aina yake. Umezidi unyakuzi wa ardhi ya Mau Mau baada ya uhuru,|” alisema Bw Nyoro.

Wakili Irungu Kang’ata anayegombea kiti cha ugavana kaunti ya Murang’a pia aliunga kuanzishwa kwa uchunguzi huo.

  • Tags

You can share this post!

Guendouzi sasa mali rasmi ya Marseille

Washirika wa Ruto na Kuria wazozana kuhusu kampeni

T L